Mikusanyiko yaendelea bila barakoa

NA HUSNA MOHAMMED

WAKATI Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zikiwa ziko katika wimbi la tatu la mripuko wa virusi vya Corona, hamasa ya kujikinga na janga hilo bado iko chini ikilinganishwa na wakati nchi hiyo ilipokumbwa na wimbi la kwanza na lile la pili.

Mtizamo huo unaonyeshwa na watu wa makundi mbalimbali ambao kwa Nyakati tofauti wamesema kuwa hamasa ya kujikinga na wimbi la kwanza la COVID – 19 na lile la pili ilikuwa kubwa ikilingishwa na sasa.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti watu kutoka katika makundi mbalimbali hapa Zanzibar, wanasema kuwa hamasa ya kujikinga na janga hilo la Covid-19 katika wimbi la tatu inaonekana kuwa ndogo huku baadhi ya watu wakionekana kutokuchukua tahadhari zinazoelekezwa na wataalam wa afya.

WANAVYOZUNGUMZA WANANCHI

Asha Mussa Mshangama mkaazi wa Mwera, anasema hali anayoiona hivi sasa ni tofauti na mripuko wa kwanza na ule wa pili.

“Ule mripuko wa kwanza na wa pili tulikuwa tunaogopa sana lakini hivi sasa tunaona kama kawaida kwa sababu hata kwenye madaladala tunaingia bila hata watu kuvaa barakoa”, alisema.

Aidha alisema katika mripuko wa awali ilikuwa lazima mtu avae barakoa, lakini sasa hakuna agizo hata moja linalolazimisha, unategemea mtu atafanya nini kwa sababu wewe ukivaa inakuwa kama kituko”, alihoji.

Nae Sophia Mkinga mkaazi wa Kibondemzungu, anasema kuwa hivi karibuni alisafiri kutoka Dar es Salaam ambapo alisema ni lazima kwenye boti kuvaa barakoa.

“Unaona hili ni agizo kutoka mamlaka husika lazima tu utavaa barakoa, hata Dar baadhi ya ruti za mabasi lazima uvae barakoa kwenye usafiri wa umma nashangaa huku bado watu wanapuuza kuhusu ugonjwa”, alisema.

WALIMU WA SKULI, MADRASA

Nao baadhi ya walimu wa skuli waliozungumza na gazeti hili, walisema kuwa ni vyema na wao wakapatiwa chanjo hasa kwa kuwa hukutana na watu wengi kwa wakati mmoja.

“Kama mimi tukiambiwa tayari kuchanjwa basi nitakuwa wa mwanzo kutokana na kazi yangu, lakini kwa sasa navaa barakoa nikitoka kwangu nikifika huku sivai”, alisema mwalimu mmoja wa Skuli ya Mambo sasa aliejitambulisha kwa jina moja la Salama.

Mwalimu mwengine wa Skuli ya Juba Islamic ambae hakupenda kutajwa jina lake, yeye anasema kuwa wameweka utaratibu wa wanafunzi kuvaa barakoa ingawa si kwa muda wote.

“Wanafunzi wetu hasa hawa wa sekondari wanavaa barakoa na hawa wanaokaa kambi ndio kabisa wasiovaa tunawarejesha na sisi walimu sote tunavaa barakoa, pia wanafunzi wote hata wa chekechea lazima wanawe mikono tumeweka pale matangi yenye mifereji wakiingia na kutoka wananawa mikono tangu lile wimbi la kwanza”, anasema Mwalimu huyo wa Juba.

NYUMBA ZA IBADA

Sheikh Abdul kadir Omar wa Masjid Taqwa wa Fuoni Mikarafuuni, anasema kuwa bado waumini hawana mwamko wa kuvaa barakoa wala kukaa mbalimbali katika safu.

“Tofauti na lile wimbi la kwanza tulikuwa na mwamko sana juu ya kinga dhidi ya corona lakini hivi sasa kama si huku kutia udhu msikitini basi wengi wangekuwa hata mikono hawanawi kwa sababu hatujaweka ndoo za kunawia mikono”, alisema Sheikh huyo.

Alifahamisha kuwa, wakisali wanakaa kama kawaida na wala si kama awali wa wimbi la kwanza, ila anasema kuwa baadhi ya wakati hukumbushana angalau kwa muda mchache juu ya kujikinga na corona.

Nae Padri wa Kanisa Anglican Zanzibar, Godwin Emmanuel Masoud, alisema waumini wa kanisa hilo wana maamuzi yao ya jinsi ya kujikinga na corona.

“Sisi kama kanisa hatujamkataza wala kumlazimisha muumini kuvaa barakoa au kuchanja corona na kwa kuwa ni hiari ya mtu basi kama atafanya anavyotaka sawa”, alisema.

Aidha alisema kuwa kama wao viongozi wa kanisa wanaaminika, bado wanaendelea kutoa taaluma juu ya kinga ya corona na wataendelea kufanya hivyo kusudi kuona hakuna maambukizi kwa waumini wa kanisa hilo.

“Tunaendelea kutoa taaluma na ndio maana tangu wimbi la kwanza tumeweka ndoo za maji ili watu kunawa mikono pamoja na vitakasa mikono na tutaendelea kufanya hivyo kwani dini pia inataka usafi wa mwili na wa kiwiliwili”, alisema Padri huyo.

Anasema hadi sasa hakuna muumini hata mmoja wa kanisa hilo alieugua corona jambo ambalo linasaidia pia wakati wanapotoa tahadhari.

Kwa upande wake Ustadhi Omar Khalfan wa Madrasatul Munawar ya Amani kwa mabata, anasema kuwa katika madrasa yao kuna wanafunzi wapatao 200 na wote hawavai barakoa.

Tunao wanafunzi makundi matatu wa kijuzuuni, msahafuni na waliohitimu wanawake na wanaume tunawaweka makundi matatu tofauti, wote hawavai barakoa, ni Mung utu anaetulinda”, alisema.

Alisema inakuwa ni vigumu kuvaa barakoa na ndio maana kile kipindi cha wimbi la kwanza madrasa zilifungwa na sasa wanafunzi wanaendelea kukaa pamoja tofauti na wimbi la kwanza angalau kabla madrasa hazijafungwa na zilipofunguliwa tukiwaweka kwa hatua kidogo.

VIWANJA VYA MICHEZO NA BURUDANI

Kama ilivyo maeneo mengine lakini imebainika kuwa kwenye viwanja vingi vya michezo kumekuwa na tahadhari ndogo juu ya ugonjwa huo.

Akizungumza na makala haya, kamisaa mmoja wa mchezo wa mpira wa miguu, ambae hakutaka kutajwa jina lake kwa madai si msemaji, anasema kuwa wachezaji wa mpira hasa wa viwanja vya Mao ndani na Amani wanavaa barakoa wanapoingia kattika vyumba.

“Wanakuja na barakoa zao wakifika wanavua na maji ya kunawa mikono tumeweka milango yote hata mashabiki nao wanatakiwa kunawa”. Alisema.

Hata hivyo, alikiri kuwa bado kuna changamoto kubwa na kwamba watu wengi hata hao mashabiki wanaona kama ni hiari kujikinga, huku wakisahau kuwa mkusanyiko ni moja ya njia ya maambukizi ya corona.

WAHUDUMU WA AFYA WANAZUNGUMZIAJE KUHUSU UVAAJI BARAKOA

Nao wahudumu wa afya wakizungumza na makala haya wanasema kuwa wanalazimika kuvaa barakoa muda wote wakiwa kazini.

Wakizungumza huko hospitali ya rufaa Mnazi mmoja, walisema kuwa tangu wimbi la kwanza la ugonjwa wa corona wanaendeleza kuvaa barakoa hadi sasa.

“Unajua sisi ni lazima kuvaa barakoa tangu hata kama haijaja corona kutokana na kazi zetu kwani mbali ya ugonjwa wa corona lakini kuna maambukizi ya kifua kikuu, homa ya ini na magonjwa mengine hii barakoa inasaidia sana”, alisema muuguzi mmoja.

Afisa Muuguzi Mwandamizi wa kitengo cha chanjo ya corona katika hospitali ya Mnazimmoja, Mwanahawa Ngwali Ahmeid, alisema yeye analazimika kuvaa barakoa n ahata mpira wa mikono ‘glavu’ kwa baadhi ya wakati kwa kuwa kazi yake inamtaka kufanya hivyo.

“Barakoa ni lazima hii ni hospitali kuu hata wanaokuja kuangalia ugonjwa hapa umewekwa utaraibu watu wavae barakoa seuze sisi muda wote tunaowahudumia wagonjwa”, alisema.

Nae Daktari bingwa wa kitengo cha masikio, pua na koo katika hospitali hiyo ya Mnazi mmoja, Dk. Khalid Yussuf Alawi, anasema kwa kuwa barakoa ni moja ya kinga dhidi ya corona haoni umuhimu wa kutovaa barakoa.

Alisema ugonjwa wa corona upo na jamii haipaswi kudharau na kwamba serikali kuleta chanjo na kutoa taaluma ya kujikinga ni moja ya kuwalinda raia wake.

“Kama wako wanaochukulia rahisi shauri zao tunajua ugonjwa upon a kama wale ambao hawajapata chanjo lazima wachukue tahadhari ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa”, alisema.

Aliwataka wananchi kuacha dharau na kusema kuwa mikusanyiko mingi kama maziko, shughuli ya harusi n ahata michezo bado wananchi hawajaona umuhimu wa kujikinga na corona.

Nae Issa Khamis Ali, ambae ni Afisa muuguzi msaidizi, alisema kuwa licha ya kumaliza dozi ya chanjo ya corona lakini pia anavaa barakoa.

Alisema kuwa ingawa chanjo ya corona ni hiari, kuvaa barakoa ni hiari lakini pia jamii haipaswi kupuuza kwa kuwa itawasaidia kujikinga na corona.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii nchini Tanzania, wanasema Watanzania wanapaswa kujifunza katika wimbi la kwanza na la pili ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari kubwa katika kupambana na vita hii inavyoonekana kuwa pasua kichwa ulimwenguni kote.

Akizungumza na Gazeti hili, Mkuu wa Kitengo cha Kinga, katika wizara hiyo, Halima Ali Khamis, alikiri kutokuweko kwa tahadhari hasa wananchi kwenye shughuli mbalimbali za kijamii.

“Angalau kwenye shughuli za kiserikali utaona watu wanavaa barakoa lakini kwenye shughuli kama michezo, harusi, mazishi hakuna tahadhari hata moja inayochukuliwa”, anasema.

“Hawa wenye maradhi kama saratani, moyo, pumu, kisukari na magonjwa mengine makubwa tunawashauri wavae barakoa hata kama watapata chanjo kwani barakoa ni moja ya kinga”, alisema Halima.

Hata hivyo, alisema kuwa wakati wowote kuanzia sasa wataanza kurusha na kutoa vipindi maalumu kupitia vyombo vya habari namna ya watu kuchukua tahadhari na kujikinga na wimbi hili la tatu baada ya kuona masharti yamelegezwa.

Kuhusu chanjo, Mkuu huyo wa kitengo aliongeza kuwa Sambamba na makundi hayo lakini pia alisema wanakusudia kutoa chanjo hiyo kwa wafanyakazi wanaohudumia watu wengi kama walimu wa skuli na madrasa, viongozi wa dini kwa maana misikiti na makanisa, mabenki, uwanja wa ndege, bandarini, mahospitalini zoezi ambalo linaendelea kufanyika kwa ustadi mkubwa.

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na watoto, Nassor Ahmeid Mazrui, alisema kwa sasa Serikali kupitia wizara hiyo imeanza kutoa chanjo ya corona kwa makundi maalumu ambayo ni hatarishi zaidi kuambukizwa ugonjwa huu ambayo ni pamoja na wafanyakazi wa milango mikuu ya kuingia nchini (Viwanja vya ndege na Bandarini).

Aliyataja Makundi mengine ni waongoza watalii, madereva wanaosafirisha wageni na watalii, wafanyakazi wa vyombo vya usafiri vya ndani na nje ya nchi, wafanyakazi wa mahoteli, wazee kuanzia miaka 55 na watu wenye magonjwa sugu na ya muda mrefu.

Kwa upande wa elimu ya afya kwa jamii, Waziri Mazrui. alisema pamoja na utoaji wa chanjo hiyo bado jamii inatakiwa kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga ugonjwa huo ili kusaidia kupunguza kujikinga na kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu hapa nchini.

Aliwasisitiza, kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo kama inavyoshauriwa na wataalamu na wizara ya Afya ikiwemo kukaa umbali usiopungua mita moja baina ya mtu na mtu, matumizi ya maji salama kwa kukosha mikono au kutumia vitakasa mikono,matumizi ya barakoa,kuepuka kupeana mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.​

Katika hatua nyengine, Waziri Mazrui, alitahadharisha jamii juu ya wimbi la nne la ugoinjwa huo linalojulikana kwa jina la Lamda ambalo limeshaanza katika nchi ya Peru na linashuka katika nchi za Marekani ya Kusini ambalo lina athari zaidi.

UKUBWA WA TATIZO LA CORONA ZANZIBAR

Hadi kufikia wiki iliyopita jumla ya watu 15 wamefariki dunia kwa ugonjwa wa corona hapa Zanzibar, huku watu 390 wakigundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo wakiwemo Watanzania 112 na wageni 278 kutoka mataifa mbali mbali duniani.

Kati ya watu hao wamo watu 29,326 waliopimwa katika vituo na hospitali mbali mbali Unguja na Pemba kuanzia Juni 25 hadi Agosti 10 mwaka huu.

Aidha watu 390 waliothibitika kuwa na maambuki ya virusi vya Corona, 207 wamepona na wanaendelea na majukumu yao na wagonjwa waliobaki ni 183 (Watanzania 32 na wageni ni 151) na wagonjwa 24 wamelazwa na wanaendelea na matibabu katika Hospitali mbali mbali hapa Zanzibar.

NINI UGONJWA WA CORONA

Ugonjwa wa Virusi vya Corona (Cov) ni familia ya virusi vinavoysababisha ugonjwa kuanzia mafua ya kawaida hadi magonjwa makali zaidi kama vile matatizo ya kupumua (MERS-CoV) na SARS-CoV.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO) lilisema kuwa ugonjwa wa virusi vya Corona vya COVID-19 ni mripuko mpya uliogunduliwa mwaka 2019 na havikuwahi kubainika hapo kabla miongoni mwa bindamu.

Dalili zake ni pamoja na homa, kikohozi, shida katika kupumua, na katika hali ngumu zaidi, maambukizi yanaweza kusababisha, nimonia, kukosa pumzi, kushindwa kufanyakazi kwa figo na hata kifo.

Aidha WHO lilisema kuwa hadi kufikia mwezi uliopita wa Julai zaidi ya watu milioni 4 wamefariki kwa ugonjwa wa corona huku watu wapatao milioni 183,934,913 wakiougua ugonjwa huo.

Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na wimbi la tatu la Covid-19 hivi sasa huku Serikali zote mbili zikionekana kuchukua hatua ikiwemo kuwachanja wananchi wake walio tayari kuchanjwa.