NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, amemtaka Mwenyekiti wa Baraza la Skuli ya Sheria kuzingatia na kufuata sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ili kwenda sambamba na matakwa ya nchi.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Mwenyekiti wa baraza, Mkuu wa skuli na wajumbe wa baraza la Skuli hiyo aliowachagua hivi karibuni, ofisini kwake Mazizini nje kidogo na mji wa Zanzibar.

Alisema, sheria ni msingi mkubwa wa kuendeleza maslahi ya nchi hivyo skuli hiyo ina jukumu la kuendeleza sheria zilizowekwa kwa mustakbali wa Zanzibar na watu wake.

Alisema, endapo wajumbe hao na watendaji wa taasisi hiyo, wataiendesha skuli hiyo kama inavyostahiki na kutoa watu wenye sifa watakaoipunguzia mzigo serikali kwa kutatua changamoto zilizopo kwa haraka.

Aidha Waziri Haroun, alisema serikali imeamua kuanzisha chuo hicho, kwa lengo la kusaidia wananchi, hivyo ni vyema kuandaa mafunzo pamoja na programu maalum ambazo zitakidhi mahitaji ya nchi.

Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Skuli ya Sheria, Mbarouk Salim Mbarouk, aliiomba wizara kulifanyia kazi suala la kukabidhiwa majengo ofisi katika Nyumba za wazee, Sebleni na kuharakisha upatikanaji wa wafanyakazi wa kada mbali mbali.

Alieleza kuwa kupatikana kwa watendaji wenye weledi wa kada husika, kutakamilisha rasimu ya muundo wa skuli hiyo kwa haraka.

Aidha aliwashukuru watendaji wa skuli ya sheria kwa juhudi walizochukua za kuhakikisha chuo hicho kinasonga mbele na kuleta maendeleo ya sekta ya sheria pamoja na kuhakikisha kesi za udhalilishaji zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka.