Abaini mafuta, mchele uliopitwa na wakati

NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ametoa siku 10 kuanzia jana kuangamizwa ama kurejeshwa zilikotoka bidhaa zilizoingizwa nchini ambazo zimethibitika kupitwa na muda wa matumizi.

Hemed alitoa agizo hilo huko Bandarini Malindi Mjini Zanzibar wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea baadhi ya maghala.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili alibaini kuwepo kwa ghala lililohifadhi mafuta lainishi (oil) ambayo yaliingizwa nchini mwaka 2019 kutoka Dubai na kukosa kiwango kwa matumizi ya vyombo vya moto.

Alisema ni vyema kwa wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kuhakikisha Zanzibar haipokei bidhaa zilizopitwa na wakati kwa usalama wa wananchi na kuitaka wizara hiyo kuchukua hatua kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa zilizopitwa na wakati ili iwe fundisho kwa wengine.

“Zanzibar siyo sehemu ya kutupa bidhaa zisizo salama, naiagiza wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kuhakikisha wanachukua hatua kali kwa wahusika wanaoleta bidhaa hizo”, alisema.

Katika ziara hiyo Hemed alikagua mchele aina ya Asha Kuku ulioletwa na kampuni ya A.R.Y ulioingia Zanzibar Julai 11, mwaka huu na mchele ulioletwa na I.A SIWJE TRADERS ulioingia Zanzibar Juni 30 mwaka huu, ukiwa kwenye makontena 10 sawa na tani 260.

Hemed aliitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kumaliza kesi ya mchele wa I.A SIWJI TRADER ambapo kampuni hiyo imeashiria kutenda vitendo vya uhujumu uchumi kwa kutoa rushwa ili kuhalalisha kuingizwa nchini bidhaa iliyokwisha pitwa na muda.

Akitoa taarifa kuhusu bidhaa ya mafuta lainishi Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Viwango Zanzibar (ZBS), Mohamed Mwalim Simai alisema kuwa bidhaa hiyo ilikaguliwa na TBS na kukataliwa na hatimae muhusika huyo kuhamishia Zanzibar bidhaa hiyo ambapo ZBS imeizuia kuingia sokoni.

Kwa upande wake Mkuu wa Usajili na Tathmini ya Chakula kutoka Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA), Khadija Ali Sheha alisema mchele ulioingizwa Zanzibar na kampuni hizo umeshafanyiwa vipimo na kuonekana kupitwa na wakati sambamba na kugundulika kuwa haufai kwa matumizi ya binadamu.