NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amezitaka taasisi na jamii kuthamini kazi inayofanywa na wasanii nchini kutokana na mchango wao katika kufanikisha maendeleo ya taifa.

Hemed alieleza hayo wakati akizindua rasmi tamasha la kwanza la washairi Tanzania lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

Alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa washairi nchini kutokana na kazi yao nzuri ya kufikishia ujumbe jamii ikiwemo kupinga vitendo vya udhalilishaji, kupiga vita dawa za kulevya na kutoa elimu kuhusiana na masuala ya afya.

Alieleza kuwa mchango huo unaotolewa na wasanii ikijumuisha wasanii wa utunzi wa mashairi imesababisha serikali zote mbili kuunda wizara maalum zinazohusiana na utamaduni, sanaa na michezo katika kuhakikisha kuwa tasnia hiyo inapiga hatua.

“Washairi wamekuwa mstari wa mbele kuisadia jamii hasa katika kufikisha ujumbe katika kukemea matendo maovu, kushajiisha ustawi wa wananchi kiafya wakati wa maradhi ya miripuki ya maradhi kama vile kipindupindu, UKIMWI na hata janga la covid 19”, alisema Hemed.

Akizungumzia suala la kuhifadhi kazi za wasanii Makamu wa Pili wa Rais alizitaka jumuiya za hakimiliki COSOTA na COSOZA kusimamia vyema kanuni zilizopo za ukusanyaji wa mirabaha kutoka kwa watumiaji wa kazi za sanaa ili wasanii wanufaike na matunda ya kazi zao.

Aidha, aliyakumbusha mabaraza yanayosimamia sanaa Tanzania kuendelea kuwalea wasanii wa mashairi na sanaa nyenginezo na kuyataka mabaraza hayo kuwawekea mazingira rafiki washairi ili wafaidike na kazi zao za sanaa.

Katika hotuba yake Makamu wa Pili wa Rais aliwataka washairi kutumia mitandao ya kijamii kama vile facebook, youtube, instagram ili kuuza kazi zao na kujikwamua na ukali wa maisha.

Kuhusiana na changamoto zinazowakabili washairi hao, Hemed aliutaka uongozi wa wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha kuwa wanakaa pamoja na washairi hao ili kuzimaliza changamoto zinazowakabili.

Naye Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita aliwapongeza washairi kwa kuandaa tamasha hilo hali hiyo imesababisha kurudisha hadhi ya mashairi nchini na kuwataka washairi hao kuiga na kusoma kupitia washairi waliotangulia.

Tabia alisema kuwa jamii hunufaika kupitia kazi za washairi hasa katika kuelimisha kukosoa na kuburudisha kutokana na matumizi mazuri ya lugha ya Kiswahili katika kazi hizo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa umoja wa washairi Tanzania (UWASHATA) Hassan Ligile alisema tamasha hili litakuwa endelevu ambapo kila mwaka hali itakayosaidia kurudisha hadhi ya mashairi nchini.

Alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa wizara ya Habari Zanzibar kutokana na mchango wake mkubwa katika kufanikisha kufanyika kwa tamasha hilo na kuahidi tamasha lijalo litafanyika kupitia upande mwengine wa muungano.

Kupitia tamasha hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alizindua kazi mbali mbali za watunzi wa mashairi kutoka Zanzibar na Tanzania bara ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa jamii.