Asema 80bn/- zimetengwa kwa shughuli hiyo

NA KASSIM ABDI, OMPR

MJUMBE wa Kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM, Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali ya awamu ya nane imetenga zaidi shilingi bilioni 80 ili kutoa fursa zaidi kwa makundi mbali mbali kujiajiri kwa kuwawezesha kuwapatia mitaji kwa lengo la kujiajiri.

Hemed alieleza hayo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa mkoa wa Kaskazini Unguja katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za CCM Mkoa wa Kaskazini zilizopo Mahonda.

Alifafanua kuwa, katika kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa, Rais wa Zanzibar na Mwenyektii wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amemteuwa katibu mkuu anayesimamia kazi na uwezeshaji kwa lengo la kufanikisha azma ya serikali ya kuwawezesha wananchi wake kupitia makundi mbali mbali.

Akigusia suala la uongozi ndani ya chama, Hemed alisema CCM imeweka taratibu za kikatiba za kutafuta viongozi na kuwataka viongozi kuacha kujinadi kwa kupanga safu za uongozi na kusubiri muda ukifika chama kitatangaza taratibu zake.

Kuhusu dawa ya kulevya, Hemed aliwaomba viongozi hao kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya nane katika kupambana na kadhia hiyo ili kujenga taifa lenye watu wenye afya bora.

Alifafanua kuwa, serikali imepanga kuwachukua hatua kali ikiwemo kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria kwa lengo la kuwadhibiti wale wote wanaojihusisha na vitendo viovu vinavyoiharibu jamii.

Katika kikao hicho, Hemed aliwataka viongozi wa majimbo kuepukana na  majungu na fitina na badala yake wafanyekazi kwa kushirikiana pamoja kwa kuwashirikisha vingozi wa serikali na chama katika ngazi zote wakati wakitekeleza majukumu yao.

Hemed aliwataka viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili, miiko na misingi ya chama hicho sambamba na kufanyakazi kwa mashirikiano ili kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Aidha Hemed aliwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kushawishi jamii kuunga mkono juhudi za serikali ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2020-2025

Nae Katibu wa CCM Mkoa wa kaskaizni Unguja, Mula Othman Zubeir amemueleza Hemed kuwa Mkoa huo unasimamia vyema utekelezaji wa ilani hadi sasa kwa mashikiano ya karibu na serikali ya Mkoa.

Aidha alisema wamefanikiwa kusajili zaidi ya wanachama 25,000 kwa njia ya elektroniki kwa kutekeleza agizo la chama la kusajili wanachama kwa mfumo huo wa kisasa.

Kwa upande wao wanachama wa chama cha mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja walimuelezea Makamu huyo kuwa kumekuwepo kwa changamoto ya upatikanaji vyeti vya kuzaliwa na kukosa maji ya uhakika kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kilimo.