Ni baada ya majadiliano ya SMZ, SMT
Hati 11 zasainiwa kuondoa kero za muungano
MADINA ISSA NA TATU MAKAME
TANZANIA imeandika historia baada ya hapo jana kusaini hati za makubaliano ya kuondoa hoja 11 za muungano zilizopatiwa ufumbuzi katika kikao kilichowashirikisha viongozi wa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Miongozni mwa hoja hizo zilizopatiwa ufumbuzi na kufikiwa makubaliano ya pamoja ni uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu, mkataba wa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mpigaduri, mkataba wa mkopo wa mradi wa matengenezo ya hospitali ya Mnazimmoja na mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada kutoka nje.
Hoja nyengine zilizofikiwa muafaka ni uingizaji wa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za muungano, uingizaji maziwa kutoka Zanzibar kwenda soko la bara, usimamizi wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi kwenye huduma za simu unaofanywa na Bodi ya Mapato Zanzibar.
Nyengine ni mapato yanayokusanywa na Idara ya Uhamiaji kwa upande wa Zanzibar, Mkataba wa mkopo wa ujenzi wa barabara ya Chake chake hadi Wete Pemba.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, alisema hatua hiyo itawezesha kutungwa sheria za usimamizi bora wa bahari katika kulinda rasilimali zilizopo.
Aidha alisema utaratibu huo utasaidia kukuza harakati za uwekezaji na kuongeza ufanisi katika kutumia miradi ya maendeleo na kuimarisha huduma za afya kupitia hospitali ya Mnazimmoja.
Alisema kuondolewa kwa hoja kumetokana na majadiliano yaliofanyika kwa pande mbili za muungano ambapo kikao hicho kimefanyika Zanzibar kikiongozwa na Dk. Mpango.
Aidha alisema kuondolewa kwa hoja hizo katika muungano kutaleta faida kubwa kwa vizazi vya sasa na baadae katika pande mbili za muungano huo.
Alisema mafanikio mengine yatakayopatikana ni kuimarisha uchumi na kuondoa usumbufu kwa wananchi na kuendelea kushikamana, kushirikiana na kujenga umoja wao.
Sambamba na hayo, aliwataka mawaziri wa serikali zote kuzipatia ufumbuzi hoja za masuala ya fedha ambazo hazipatiwa ufumbuzi ili pande zote mbili zinufaike na mgao wa fedha za muungano.
Nae, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, alisema muungano wa Tanzania ni nguzo muhimu kwa taifa, hivyo kusainiwa kwa makunaliano ni matukio chanya ya vikao kati ya serikali mbili.
“Kusainiwa kwa hati za makubaliano haya kuna faida kubwa na itasaidia kuondosha migongano, manung’uniko na malalamiko kwa vizazi vya sasa na vya baadae na kupata maendeleo”, alisema.
Aidha alifahamisha kuwa makubaliano hayo yatawajengea imani wananchi kutatua changamoto zinazowakabili ambazo zilikua zikiwakwanza kutokana na hoja hizo kabla ya kuondolewa katika masuala ya muungano.
“Kuna baadhi ya watu walitaka muungano huu uvunjike kwa madai ya upande mmoja wa muugano kufanya maamuzi bila ya makubaliano, lakini ilani ya CCM inasisitiza uimarisha wa muungano”, alisema.
Sambamba na hayo, alisema makubaliano hayo yataleta faida nyingi ikiwemo kuondosha migongano na malalamiko kwa vizazi vya sasa na baadae kwa maendeleo endelevu pamoja na kunufaisha wawekezaji na wafanya biashara kwa pande hizo za muungano.
Pamoja na hayo, alisema kuwa vikao na shughuli kama hizo zinathibitiisha kuwa maamuzi yote yanayototolewa ni makubaliano baina ya pande hizo mbili, hivyo, aliwataka wananchi wawe wanafuatilia kwa katibu shughuli hizo ili kuondosha sintofahaamu zisizo za lazima.
Kwa upande wake waziri mkuu, Kassim Majaliwa Majaaliwa, alisema kusainiwa na kukubaliwa kwa hoja hizo wananchi wataendelea kuendesha shughuli zao kwa amani na utulivu.
Mapema kaimu waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa rais, Sera na Uratibu na Baraza la wawakilishi, Saada Mkuya Saada Mkuya Salum na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Seleiman Said Jafo, walisema hatua hiyo imetokana na maagizo ya viongozi wakuu.
Hivyo waliwataka watendaji kufanya kazi kwa kuzingatia mikataba hiyo pamoja na kufanya tathmini ili kuona utekelezaji wake unaleta manufaa kwa pande zote.