Itahusisha jengo la ghorofa 70
NA SALUM VUAI
ZANZIBAR inatarajia kuandika historia mpya katika sekta ya utalii kupitia dhana ya uchumi wa buluu kwa kuingia kwenye uwekezaji mkubwa wa hoteli ya aina yake itakayokuwa na ghorofa 70.
Kampuni ya kitanzania AICL Group imeingia makubaliano na kampuni ya xCassia yenye utaalamu na uzoefu wa kusanifu na kuchora ramani za majengo marefu duniani kupitia uongozi wa Edinburgh Crowland Management Ltd yenye ofisi zake katika majiji ya New York na Dubai.
Ujenzi wa hoteli hiyo ya kwanza ya aina yake Afrika Mashariki na Kati utafanyika katika kisiwa cha Chapwani kwa eneo la ukubwa wa hekta 20, kilomita 15 kutoka Mji Mkongwe ulioko kwenye urithi wa kimataifa chini ya Shirika la UNESCO.
Aidha, hoteli hiyo itakayokuwa na aina mbalimbali za huduma ukiwemo ukumbi mkubwa wa mikutano utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 1,000 na zile za burudani, itasarifiwa katika eneo la mita za mraba 370,000.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini, mkurugenzi mkuu na msanifu wa kampuni ya xCassia Jean-Paul Cassia alisema kuwa alitamani kuanza mradi huo zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Alisema kutokana na ukubwa na upekee wake, ilichukua zaidi ya miaka 15 ya vikao, safari za majadiliano, kukubali kutokukubaliana, tafiti za mazingira na mambo ya msingi kabla kutimia kwa azma hiyo mapema mwaka 2021.
“Mradi huu ulikuwa na mambo yote na alama ambayo mtu yeyote angependa kuufanya lakini kilichokosekana ni mwekezaji sahihi mwenye dira na eneo la kuifanya ndoto hii iwe kweli”, alisema Jean-Paul.
Alifahamisha kuwa, mwanga wa matumaini ulianza kuonekana mwaka 2019 na 2020 baada ya waendelezaji wawili mahiri nchini Vietnam na Saudi Arabia, kuipa kazi kampuni ya xCassia kuandaa utafiti kwa ajili ya kuingiza mchoro katika mpango mkuu wao.
“Pamoja na maumbile na changamoto zake kama urefu wa jengo, bajeti, bahari na upatikanaji wa miundombinu, sambamba na mripuko wa Covid 19, hii ilikuwa fursa adhimu kwetu kwani mapema 2021 tuliitwa na Mwenyekiti Mtendaji wa AICL Group Yussuf Amour ambaye ana shauku kubwa kufanya kitu kitakachokuwa alama kwa nchi yake Zanzibar.
Naye Mkurugenzi Mipango na Maendeleo wa AICL Group Emmanuel Umoh, alisema pamoja na mambo mengine, lengo la mradi huo ni kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuleta maendeleo kupitia uchumi wa buluu kama ilivyo azma ya Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Alisema hoteli hiyo itakayoitwa ‘Zanzibar Domino Commercial Tower’, itajitengeneza kuwa kati ya alama na vituo vikuu vya utalii, starehe, utamaduni na mikutano ya kimataifa barani Afrika, itawapa wageni, wenyeji na fursa nyingi za kujiinua kibiashara na pia itakuwa kigezo kwa wawekezaji wengine kufikiria uanzishaji wa miradi mikubwa kama hiyo.
Alisema ujenzi wa hoteli hiyo utakaofanyika kwa awamu tofauti ukikadiriwa kuchukua miaka minne na nusu hadi kukamilika kwake unatarajiwa kutoa ajira mbalimbali kwa wazanzibari na watanzania kwa jumla na kuiingizia kodi serikali.
Aidha, utahusisha ujenzi wa daraja litakalotumika kutoa huduma zote za msingi ikiwemo upakizi, ambapo kituo cha kisiwa kilichotengenezwa kitakuwa umbali wa kilomita 1.5 kutoka barabara kuu ya mwambao ambacho pia kitatumia kupokea vyombo vya baharini, zikiwemo mashua zinazobeba watalii.
Umoh alisema ujenzi huo utahusisha villa 104 juu ya maji zikiwa na ukubwa kati ya mita za mraba 360 hadi 500, zikipangiliwa kwa namna tafauti pamoja na vituo vya huduma nyengine mbalimbali za kihoteli na mikahawa, huku akieleza kuwa dola bilioni 1.3 zimetengwa kuanza hatua za awali.
Akizungumza baada ya utiaji saini makubaliano hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Soraga, alisema mradi huo ni hatua muhimu katika kufungua njia kwa wawekezaji wageni na wazalendo wenye nia ya kuweka vitega uchumi vyao hapa nchini.
Aliwahakikishia kuwa, serikali imejidhatiti kuibadilisha Zanzibar na kuinua ustawi wa watu wake kiuchumi, hivyo hawatakuwa tayari kusikia wanawekewa vikwazo au urasimu wa aina yoyote utakaolenga kukwamisha mpango huo.
Hafla hiyo ilishirikisha watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali, ikiwemo Mamlaka ya Usafiri wa Baharini, ambapo mwakilishi wake Msilimiwa Idi Juma, alisisitiza umuhimu wa kuepuka uharibifu wa mazingira na kuweka miundombinu ya kukabiliana na matukio hatarishi yanayoweza kutokea ha