JUBA, SUDAN KUSINI
JUMUIYA ya ushikiriano wa maendeleo ya nchi za mashariki mwa Afrika IGAD imezitaka pande za kijeshi zinazohasimiana za vuguvugu la Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar kufungua njia ya mazungumzo baada ya mapigano makali kuzuka mwishoni mwa wiki.
Karibu watu 30 waliripotiwa kuuawa katika makabiliano yaliyozuka Jumamosi, siku chache tu baada ya mahasimu wa Machar katika chama chake cha upinzani cha SPLA-IO kusema walimuondoa kama kiongozi wa chama na mkuu wa majeshi yake.
IGAD iliitisha mkutano wa dharura wa mawaziri wake wa mambo ya kigeni, ikisema hali ya sasa ya kisiasa katika taifa hilo changa inahitaji kushughulikiwa kwa haraka na baraza hilo.
Katibu Mkuu wa IGAD Workneh Gebeyehu aliyataka makundi ya SPLM na SPLA-IO kufanya mazungumzo ya kutatua tofauti zao kwa njia ya amani ili kulinda utekelezwaji wa makubaliano ya azimio la mzozo wa Sudan Kusini.