NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Tanzania, limetoa onyo kwa mtu ama kikundi cha watu kitakachojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au maandamano kwa lengo la kushinikiza mahakama kumuachia mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Mbowe alikamatwa mkoani Mwanza akiwa na wafuasi 15 wa CHADEMA kwa kutoa matamshi yenye kuashiria uvunjifu wa amani ikiwemo kuhamasisha na kushajiisha wananchi kwa vitisho na sharti kuwa lazima katiba mpya ipatikane.

Baada ya kukamatwa Mbowe alipelekwa jijini Dar es Salaam ambapo kulikuwa na kesi inayopelelezwa dhidi yake kuhusiana na kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi.

Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari jana mkuu wa jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, alisema tuhuma zote kwa sasa zipo chini ya mamlaka ya mahakama na kwamba muhimili huo haupaswi kuingiliwa katika kutekeleza majukumu yake.

Alisema suala la dhamana kwa kesi inayomkabili Mbowe na viongozi wengine wa CHADEMA ni kujumu la kisheria na linasimamiwa na mahakama, hivyo jeshi la polisi halitegemei mtu wala kikundi cha watu kwa namna yoyote kutoa shinikizo.

“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa mtu ama kikundi cha watu kitakachojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana kwa namna yoyote ile kwa lengo la kushinikiza mahakama kumuachia mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Aikael Mbowe”, alisema Sirro.