NA AMEIR KHALID

RAIS wa India Shri Ram Nath Kovid amezitakia jamii zote za kihindi zinazoishi nje ya India kheri ya siku ya uhuru wa taifa hilo.

Akitoa salamu za siku ya uhuru wa nchi hiyo hapa Zanzibar kwa niaba ya Rais Ram, Balozi mdogo wa India aliyepo Zanzibar, Bhagwant Singh katika maadhimisho ya miaka 75 tangu kupata uhuru kwa taifa hilo alisema siku hiyo ni adhimu kwao.

Alieleza kuwa siku hiyo imetokana na waasisi wa taifa hilo kujitolea maisha yao ili kuhakikisha kizazi cha taifa hilo kinajitawala wenyewe, hivyo hana budi kutoa heshima kubwa kwa uzalendo uliooneshwa na waasisi waliofanikisha uhuru wa India.

“Taifa letu ni kama mataifa mengine mengi tu, tumeteseka kutokana na kukosa haki pamoja na kudhulimiwa kutokana na sheria za kigeni, jambo ambalo liliitenganisha India, na hiyo ndio sababu ya kuanzisha harakati za kiukombozi kwa taifa letu ziliongozwa na mwanaharakati Mahatma Gandhi, ambazo zilikuwa katika misingi ya ukweli na amani,” alisema.

Rais Kovid alisema  wakiangalia nyuma miaka 75 iliopita ya safari ya kuliunganisha taifa katika kujitawala, wana kila sababu ya kujisifu kutokana na safari ndefu ya kujipatia uhuru ambapo kwa sasa dunia inaiangalia India kama nyumbani kwa tamaduni na demokrasia ilio safi.

Aliongeza  kuwa katika tukio la hivi karibuni la michezo ya Olimpiki iliofanyika huko Tokyo, wanamichezo wa taifa la India, walioshiriki michezo tofauti wamejenga heshima kubwa kwa taifa lao kwa miaka 121 ya ushiriki wa taifa la India kwenye mashindano hayo.

Aliongeza kuwa katika sekta nyengine kama ya elimu ya juu, nguvu za jeshi, kizazi cha taifa la India kimekuwa kikifanya vyema, jambo ambalo linaifanya India kuona hatua ya maendeleo miaka ijayo.

Kutokana na changamoto ya wimbi la pili la maradhi ya Corona linalowakabili mataifa mengi duniani, rais huyo wa India alisema ni wazi janga hilo limetetemesha miundombinu ya nchi hiyo, kiasia ya kwamba miundombinu na ukuaji wa kiuchumi vyote vimeathirika kwa kiasi kikubwa, ila amesisitiza kuwa India inafanya juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa inalitafutia ufumbuzi.

Hata hivyo alieleza kuwa Serikali ya India ikishirikiana na sekta binafsi za afya pamoja na mataifa ya nje, wameweka juhudi katika kutoa misaada kama vile vifaa tiba, chanjo na dawa jambo ambalo alisema linayafanya mataifa yote duniani kuwa kitu kimoja katika kusaidia.