NEW DELHI, INDIA

INDIA inapeleka mwezi huu jeshi la wanamaji katika Bahari ya Kusini mwa China ili kuimarisha mahusiano yake ya usalama na nchi rafiki.Hatua hiyo inayoashiria nia yake ya kuwa na jukumu kubwa katika juhudi za kikanda za kupambana na China.

Jeshi la India tangu jadi limekuwa likihofia kuichokoza China lakini hali imebadilika kufuatia makabiliano ya mwaka jana kati ya wanajeshi wa nchi hizo kwenye mpaka unaogombaniwa.

Makabiliano hayo yaliisukuma India kujiweka karibu na Marekani dhidi ya China.

Taarifa ya jeshi la wanamaji la India ilisema meli nne ikiwemo manowari ya kufyatua makombora zitapelekwa kwa kipindi cha miezi miwili katika eneo la Kusini mashariki mwa Asia, Bahari ya Kusini mwa China na Magharibi mwa Pasifiki.

Meli hizo za India zitakuwa sehemu ya luteka za pamoja za kijeshi za kila mwaka zinazozishirikisha Marekani, Japan na Australia kwenye pwani ya Guam.