TEHRAN, IRAN

IRAN imekanusha madai kwamba imehusika katika shambulizi linaloshukiwa kufanywa kutumia ndege inayoendeshwa bila rubani dhidi ya meli ya kibiashara yenye mahusiano na Israel katika ghuba ya Oman lililosababisha vifo vya wafanyakazi wawili.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh alisema Iran ililaani madai hayo yasiyo na msingi kutoka kwa Israel, akisema utawala wa taifa hilo ulisababisha machafuko na hali ya wasiwasi.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Yair Lapid awali aliinyoshea kidole cha lawama Iran kwa shambulizi hilo la mwishoni mwa wiki iliyopita akiandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba Iran sio tatizo la Israel, bali pia ni msafirishaji wa ugaidi, uharibifu na uyumbishaji unaowaathiri wote.

Marekani na Uingereza ziliungana na Israel kuilaumu Iran kwa hujuma hiyo, huku Marekani ikiapa kuchukua hatua stahiki.