KUALA LUMPUR, MALAYSIA
ISMAIL Sabri Yaakob wa Malaysia ameapishwa kama waziri mkuu wa tisa wa nchi hiyo hapo jana Jumamosi, akimaliza wiki ya machafuko ya kisiasa yaliyomlazimisha mtangulizi wake kujiuzulu wakati wa dharura ya kiafya inayoendelea kwa sababu ya janga la COVID-19.
Ismail Sabri ni mwanasiasa mkongwe kutoka chama tawala cha muda mrefu nchini United Malays National Organisation (UMNO), lakini wadadisi wanasema yeye ni kiongozi anaeweza kuziba pengo lililoachwa na mtangulizi wake wa muda mrefu.
Kiongozi huyo wa miaka 61 aliteuliwa kuwa waziri mkuu Ijumaa baada ya kuanguka kwa utawala wa Muhyiddin Yassin wiki hii. Yeye ni kiongozi mpya wa tatu wa Malaysia katika kipindi kisichozidi miaka minne.
Ismail Sabri anatoka kwa UMNO, chama kikuu katika umoja ambao ulitawala Malaysia kwa miongo kadhaa baada ya uhuru kutoka kwa Uingereza, ambapo
alijizolea umaarufu mkubwa wakati wa utawala wa Muhyiddin wa miezi 17.
Akiwa waziri wa ulinzi, alitoa taarifa za kila siku juu ya vita dhidi ya janga la coronavirus na alipandishwa cheo kuwa naibu waziri mkuu katika siku za mwisho za utawala.