YERUSALEMU, ISRAEL

ISRAEL imefanya mashambulizi ya anga kwa kuyalenga maghala na vituo vya mafunzo vinavyotumiwa na wapiganaji wenye muungano na Iran katika eneo la magharibi mwa Syria.

Shirika linalofuatilia Haki za Binadamu nchini Syria limesema ndege za Israeli zimeyashambulia maeneo yanayotumiwa na kundi la Hezbollah kwenye kitongoji cha Qara kinachopatikana karibu na safu za milima ya Qalamoun kwenye mpaka kati ya Syria na Lebanon.

Taarifa hizo zilithibitishwa pia na jeshi nchini Syria ambazo zilieleza kwamba ndege za Israeli zimefanya uchokozi kwa kuyalenga maeneo jirani na mji mkuu, Damascus na jimbo la Homs.

Taarifa iliyorushwa na kituo cha televisheni cha Syria ilisema  mifumo ya ulinzi ya Syria iliyazuwia baadhi ya makombora ya ndege za Israeli.

Mashambulizi ya Israel nchini Syria yanaonekana kuwa juhudi za kuizuia Iran ambayo ni mshirika mkubwa wa serikali mjini Damascus, dhidi ya kuimairisha ushawishi wake wa kijeshi kwenye kanda hiyo.