NA MADINA ISSA

MRATIBU wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, amesema kupeleka mahakamani madai ya haki kunapotumiwa vyema, kutapunguza madai ya haki kwa njia ya maandamano.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya Mawakili na Wanasheria wa Zanzibar, yaliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi, Unguja, alisema, sekta ya sheria ni pana na ina mchango mkubwa katika kutetea haki za wananchi.

Alisema kuna baadhi ya kesi zinahitaji kufanyiwa kazi kubwa na mawakili wanapaswa kuzisimamia hasa zile ambazo zinajumuisha watu wengi katika masuala ya haki za binadamu.

Naye, Meneja Programu wa American Bar Association Rule of Law Initiatives, Afrika ya Mashariki, Violah Ajok, alieleza kuwa amefurahishwa kufika Zanzibar na kushuhudia mawakili wenye uwezo mkubwa wa kuendesha kesi zenye maslahi kwa umma na kuwahimiza kuendelea kujifunza ili kuitumikia jamii kujua na kutetea haki zao.

Kwa upande wake Rais wa Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Hassan Kijogoo Corneli, alisema mawakili wa Zanzibar wanaochukua kesi za umma ni wachache sana, ikilinganishwa na wanaotetea watu binafsi na taasisi.

Hivyo alisema mafunzo hayo yataongeza wingi wa mawakili wa kuchukua kesi za haki za binaadamu na kwa kuzingatia hivi sasa wananchi wengi wanajua haki zao na kuzidai kupitia mahakama.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kituo cha Huduma na Sheria Zanzibar (ZLSC), Jamila Masoud Khamis, alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwapa nguvu na ujasiri mawakili katika utatuzi na upatikanaji wa haki zenye kuwajumuisha wananchi.

Nao baadhi ya Mawakili na Wanasheria waliopatiwa mafunzo hayo, walisema mafunzo yamesaidia kuwajengea uwezo kwa sababu wana kazi kubwa ya kuwawakilisha wananchi mahakamani katika kesi zenye mtazamo wa kuwajumuisha watu wengi katika jamii.

Wakili kutoka Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar, Miza Haji Haji, alisema wapo tayari kuwa sehemu ya jamii hivyo, hawapaswi kujitenga ambapo wanapaswa kufahamu matatizo ya jamii.