TOKYO, JAPAN

JAPAN itasitisha utoaji wa dozi milioni 1.63 za chanjo ya Moderna dhidi ya virusi vya corona, baada ya ripoti kuibuka kuhusu uchafuzi kwenye chupa ndogo kadhaa za chanjo hiyo.

Kampuni ya kutengeneza chanjo Takeda pamoja na wizara ya afya zilisema hayo.

Takeda ambayo ndiyo kampuni inayohusika na uuzaji pamoja na usambazaji wa chanjo ya Moderna nchini Japan ilisema imepokea ripoti za uchafu kupatikana ndani ya chupa za chanjo ambazo hazijafunguliwa.

Takeda haikutoa maelezo zaidi kuhusu aina ya uchafu uliopatikana, lakini ilisema haijapokea ripoti yoyote ya kusababisha wasiwasi wa kiafya kutokana na dozi zilizoathiriwa.

Kampuni hiyo imeongeza kuwa baada ya kushauriana na wizara ya afya, waliamua kusitisha matumizi ya dozi hizo kuanzia jana.

Tayari imeshaiarifu kampuni ya Moderna na kutaka uchunguzi wa haraka ufanywe.Kampuni ya Moderna hata hivyo haikutoa jibu la moja kwa moja kuhusu ombi hilo.