TOKYO, JAPANI

SERIKALI ya Japani inapanga kutuma ndege ya Kikosi cha Kujihami, SDF nchini Afghanistan ili kuwahamisha Wajapani zaidi na raia wa Afghanistan wanaofanya kazi katika ubalozi wake.

Wiki iliyopita Serikali iliwahamisha Wajapani wanaofanya kazi katika ubalozi huo mjini Kabul kwa kutumia ndege ya kijeshi ya Uingereza.

Maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na ya Ulinzi walielekea nchini Afghanistan kutathmini hali ya mambo nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Nje inasema raia wa Afghanistan wanaofanya kazi katika ubalozi wa Japani na familia zao, pamoja na Wajapani wanaofanya kazi katika mashirika ya kimataifa wametafuta msaada wa kuondoka nchini Afghanistan.Vyanzo vya habari katika wizara vinasema ndege za SDF huenda zikahamisha zaidi ya watu 500.