KINSHASA, DRC

JESHI la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limesema limekamata ngome ya mwisho ya muungano wa waasi katika jimbo la Hauts Plateaux mashariki mwa nchi hiyo, baada ya wiki nzima ya mapigano.

Operesheni hiyo ilianza Alhamis iliyopita baada ya shambulizi la makundi ya Makanika Twirwaneho Gumino na FNL, lililolenga kuikamata kambi ya jeshi.

Jimbo la Hauts Plateaux linaandamwa na mizozo yenye misingi ya kikabila, baina ya jamii ya Watutsi ya Banyamulenge na jamii nyengine zinazowazunguka.

Makundi ya Banyamulenge yaliongozwa na Kanali Michel Rukundo Makanika aliyelitoroka jeshi la serikali mwaka 2020.

Wakati huo huo, vyanzo mbali mbali kutoka Kongo na Marekani vimezungumzia kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani katika kambi moja iliyoko ndani ya mbuga ya wanyama ya Virunga katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Ikulu ya rais Felix Tshisekedi ilisema wanajeshi wa Marekani watashiriki katika mapambano dhidi ya waasi wa ADF.