DAMESKI, SYRIA

VIKOSI vya jeshi la Syria kwa ushirikiano na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran wamefanya shambulizi kusini mwa mji wa mpakani wa Daraa ili kuchukua udhibiti wa ngome ya mwisho inayokaliwa na upinzani kusini mwa Syria.

Wapiganaji wa upinzani walisema wamejibu shambulizi kutoka upande wa magharibi ambayo ilizingirwa na jeshi lililozuia  chakula,vifaa vya matibabu na mafuta kuingia katika eneo hilo.

Chanzo cha jeshi kilisema mapigano yalikuwa yakiendelea japo hakutoa maelezo zaidi.

Chombo cha habari cha serikali katika siku za hivi karibuni kimeripoti kuwa jeshi linapanga kuchukua udhibiti wa eneo hilo.Hakuna vifo au majeruhi yaliyoripotiwa katika mashambulizi hayo.

Jeshi la Syria linalosaidiwa na Urusi pamoja na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran mnamo mwaka 2018 liliuteka mji wa Daraa unaopakana na Jordan na milima ya Golan.