NA SALMINI SEGUMBA , TUDARCo

MASHINDANO ligi ya hisani, mpira wa Wavu kwa wanawake yametamatika katika viwanja vya Mfunzo.

Katika michezo hiyo timu ya JKU, imeibuka bingwa wa mashindano hayo ambayo yalikuwa na lengo la kufufua na kuziandaa timu kwa ligi ya mpira wa Wavu Zanzibar.

Licha ya mchezo huo kuwa mgumu kwa timu zote, lakini timu ya JKU ilifanikiwa kupata ushindi mnono wa seti 3-0 dhidi ya KVZ.

JKU walitinga fainali baada ya kuiadhibu Mwembeladu seti 3-0 katika hatua ya nusu fainali, huku KVZ wakipata ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Mafunzo.

Nayo timu ya Mafunzo ikishikilia nafasi ya tatu baada ya kupata ushindi wa seti 3-0 dhidi ya timu ya skuli ya Mwembeladu.

Mashindano hayo yalianza kutimua vumbi siku ya Jumatatu,23 Agosti yalishirikisha timu saba zilizopangwa katika makundi miwili, ambapo kundi A lilijumuisha timu za Mafunzo, Mwembeladu na KMKM, huku kundi B likiwa na timu za JKU, KVZ, Chuoni na Eagle V.