NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais Sera ,Utratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohamed, amesema Kamati za Kudumu za Baraza la Wakilishi, kuhakikisha zinasaidia kuongeza ufanisi ndani ya chombo hicho, na kuleta mageuzi ya maendeleo majimboni pamoja na kutimiza malengo ya serikali.

Waziri huyo akizungumza na Zanzibar Leo, baada ya kumaliza kikao  cha  Kamati ya Kudumu ya Viongozi Wakuu  ya Baraza la Wawakilishi ofisini kwake Vuga mjini Unguja.

Alisema utendaji kazi mzuri wenye kufatilia kwa karibu   utatuzi wa changamoto  za wananchi kuchapakazi kwa bidii, ubunifu na utekelezaji mzuri wa majukumu ya kazi kwa utasaidia kuimarisha ndoto walizoziweka katika majimbo yao.

“Lazima viongozi na watendaji tuchape kazi kwa bidii huku tukibuni mbinu sahihi za uimarishaji wa maendeleo katika maeneo yetu ya kazi, hivyo tutaweza kutimiza mipango tuliojiwekea katika mageuzi ya kiuchumi na kijamii”,alisema.

Aidha, Dk. Khalid, alisema ni wakati wa kushirikiana, katika kuongeza kasi ya kiutendaji, ili kuisaidia serikali kwenye uimarishaji wa maendeleo na kutimiza mipango yake iliyojiwekea ikiwemo ahadi za ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Alifahamisha kwamba hatua hiyo iwe sambamba na utumiaji wa elimu ya uendeshaji wa miradi waliojifunza katika mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAFU) hivi karibuni.

“Hakuna miujiza yoyote isipokuwa umoja wetu, mshikamano, na kubadilishana uzoefu  wa kiutendaji kwani  ndio utakaoleta matokeo chanya ya mabadiliko ya maendeleo hivyo ni vyema tuongeze kasi ya kufanyakazi”,alisema.

Alisema iwapo Wawakilishi watasimamia imara ilani ya uchaguzi, kutimiza ahadi, kutatua  kero majimboni pamoja na kuisaidia serikali ipasavyo, Zanzibar itaendelea kuimarika kiuchumi na hata upatikanaji wa huduma bora za wananchi ndani ya majimbo.

Waziri huyo, alisema mitazamo hiyo ya kiutendaji iwe sambamba na utumiaji wa  elimu nzuri ya uendeshaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwaelezea  wananchi   namna bora ya kuendesha miradi itakayoleta tija, manufaa pamoja na kupunguza  umasikini.