NA RAYA HAMAD, OMKR

KAMATI ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Kitaifa imeishauri serikali kuhakikisha kisiwa cha Mnemba kinatunzwa na kuendelezwa licha ya serikali kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kutoa utaratibu wa kukodishwa kwa visiwa vidogo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Hassan Khamis Hafidh alieleza hayo wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kuangalia maeneo ya hifadhi za mazingira na kushuhudia uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi na mwanadamu.

Hassan aliwataka watakaokodishwa visiwa hivyo kuwa watiifu katika kulinda na kuhifadhi mazingira ya visiwa na kuwasikiliza wataalamu ushauri wanaoutoa kwa kuhakikisha wanaufuata ili kuvilinda visiwa viendelee kuwepo kwa miaka ijayo.

Aidha baadhi ya wajumbe nao waliishauri serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, kuhakikisha maeneo yaliyochimbwa mchanga yanarudi katika uhalisia wake kwa kuotesha miti ya asili ili kuepuka athari zaidi za kimazingira.

Naye katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Omar Dadi Shajak alisema kuna kazi kubwa ya kuhifadhi mazingira kwenye kisiwa cha Mnemba na vyengine vyote vya Unguja na Pemba kutokana na uharibifu.

Shajak alisema pamoja na kukuza uchumi wa nchi pia wananchi wanaozungukwa na kisiwa cha Mnemba nao waweze kunufaika na kuona umuhimu wa uhifadhi wa kisiwa hicho ambacho ni moja kati ya rasilimali muhimu.

Naye mkurugenzi wa hoteli ya kisiwa cha Mnemba, Jonathan Braack alisema mmong’onyoko mkubwa wa fukwe hasa upande wa mashariki na kusini ya kisiwa hicho ni tishio.Jonathan alieleza baadhi ya hatua zinazochukuliwa kutatua changamoto hizo ni kuhamasisha upandaji na utunzaji wa miti ya asili katika kisiwa cha Mnemba ili kurudisha uoto wa asili.

Kutekeleza shughuli za uratibu na ufuatiliaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu, kutekeleza shughuli zilizolenga kudhibiti usambazaji, kuuza pamoja na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo kuandaa vikao vya ulinzi na usalama katika Shehia za Unguja na Pemba, kukamilisha maandalizi ya mpango wa muda wa kati wa matumizi ya Bajeti ya Ofisi.

Katika ziara hiyo kamati hiyo pia ilitembelea eneo lililokuwa likitumiwa kuchimbwa mchanga Bumbwini Pangatupu na eneo lililokuwa likichimbwa mawe kwa ajili ya ujenzi wa barabara shehia ya Kidaanzini na kisiwa cha Mnemba.