NAIROBI, KENYA
KENYA imeidhinisha chanjo ya China ya Sinopharm wakati nchi hiyo inaendelea na mapambano dhidi ya COVID-19 ikilenga makundi ya watu walio kwenye hatari.
Mkuu wa kikosi kazi cha Chanjo ya COVID-19 katika Wizara ya Afya ya Kenya Willis Akhwale, alisema bodi ya dawa ya Kenya imeidhinisha chanjo ya Sinopharm, ambayo imepitishwa kwa ajili ya matumizi ya dharura na Shirika la Afya Duniani WHO, ili kuimarisha utoaji wa chanjo unaoendelea duniani.
Akhwale alisema Kenya imeidhinisha chanjo ya Sinopharm, na ina imani na ufanisi wa chanjo hiyo kwa kuwa imethibitishwa na WHO.
Pia alisema hadi sasa Kenya imeidhinisha chanjo hiyo ya China pamoja na chanjo nyengine tatu ili kutoa chanjo kwa asilimia kumi ya watu wake kabla ya mwisho mwa mwaka huu.
Hadi kufikia jumatano, Kenya ilikuwa imerekodi maambukizi 224,400 yaliyothibitishwa, na asilimia 2.8 ya watu wazima tayari wamepewa chanjo kamili.