NAIROBI, KENYA

WAKATI Kenya ikishuhudia athari za mabadiliko ya tabia nchi kama vile uhaba wa mvua na ukame, nchi hiyo sasa inaongeza juhudu katika mazao mengine mbadala ambayo awali yalipuuzwa ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa chakula, huku mazao yaliyozoeleka yakikabiliwa na tishio.

Mahindi na mpunga ni miongoni mwa mazao makuu nchini Kenya ambayo yanazidi kukabiliwa na tishio la athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa mahindi, mvua zisizo tabirika zilivuruga uzalishaji katika miaka mitano iliyopita, ambapo zao hilo pia linakabiliwa na matishio kama vile ya magonjwa na wadudu.

Kwa upande wa uzalishaji wa mpunga nao pia unaathiriwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zisizotabirika, na kuifanya Kenya itegemee mazao yanayoagizwa kutoka Asia.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, wakulima kutoka sekta binafsi na za umma walianza kutambua muhogo kama zao litakaloongeza kasi ya uzalishaji wa chakula nchini Kenya.

Kama mahindi na mpunga, muhogo pia unalimwa na wakulima wadogo nchini humo, hivyo uzalishaji hautokuwa mgumu au kuhitaji kubadilishwa.