NA NASRA MANZI, WHVUM
WAZIRI wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amepokea shilingi 10,000,000 kwa ajili ya ufadhili wa ligi kuu Zanzibar.
Hafla hiyo ilifanyika ukumbi wa wizara hiyo Migombani, ambapo Katibu Mkuu mstaafu wa wizara hiyo Omar Hassan ‘King’, alimkabidhi waziri Tabia kiasi hicho cha fedha.
Akizungumza mara baada ya kupokea fedha hizo Tabia alisema ni vyema wahisani na wapenda michezo kuendelea kushirikiana na wizara ili kurudisha hadhi ya soka kama zamani.
Alisema Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo itahakikisha misingi,kanuni na sheria za mpira zinafuatwa ili mpira wa Zanzibar upige hatua.
Alimshukuru katibu huyo mstaafu kwa jitihada alizozichukua yeye binafsi pamoja na uongozi wa skuli ya Glorious kwa kutoa fedha hizo ili kuhakikisha ligi kuu inaimarika.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab alisema wizara itaendelea kushirikiana na wadau,wafadhili na wadhamini katika kuleta mafanikio ya mpira ili kupiga hatua ya kimaendeleo.
Nae Katibu Mkuu Mstaafu hiyo Omar Hassan ‘King’ ameipongeza wizara kwa kazi ya kukuza na kusimamia taasisi za michezo ili kuleta mabadiliko ya michezo katika nchi.
Aidha ameziomba klabu za michezo pamoja na vyama vya michezo kushirikiana pamoja, jambo ambalo litaleta ushindani na kupeleka soka mbele.