NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa mbio maalum za Mwenge wa Uhuru, luteni Josephine Mwambashi ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza thamani ya fedha zilizotumika katika mradi wa ujenzi wa skuli ya msingi Kasulu wilaya ya Ilala.

Kiongozi huyo alieleza hayo jana baada ya Mwenge wa Uhuru kufika skulini hapo na kukagua ujenzi wa madarasa yaliyopo na utekelezaji wake unaoendelea na kubaini kasoro kadhaa.

Luteni Mwambashi alisema shilingi milioni 544 zilizoelezwa kuwa zimetumika kwenye ujenzi wa skuli hiyo thamani yake hailingani na hali halisi, hivyo alikataa kuweka jiwe la msingi na kuiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi.

Mwambashi alisema Mwenge wa Uhuru umebaini makosa mbalimbali ikiwemo barua ya mapokeo ya fedha iliyopelekwa skulini hapo ambayo kwenye taarifa inaonesha shilingi milioni 555 huku barua iliyoonekana ni mapokezi ya shilingi milioni 200 na barua nyingine ya mapokeo ni shilingi milioni 300 hainekani.

Alisema fedha iliyolipwa kwa mtekelezaji wa mradi huo hadi sasa ni kiasi cha shilingi milioni 544 kwa madarasa ya chini na juu ambapo wamefanya majumuisho hati zote za malipo yaliyolipwa ili kutafuta fedha hizo.

“Tumetumia muda mrefu kwa sababu mkandarasi hajaonesha muktasari wa kiasi cha fedha shilingi milioni 544 imefanya shughuli gani, kwa hiyo wametumia muda mrefu kujumlisha hati zote za malipo ambapo inaonesha hati za malipo gharama iliyotumika ni shilingi milioni 389”, alisema.

Akifafanua kuwa ikichukuliwa kiasi cha fedha shilingi milioni 544 ukitoa shilingi milioni 389 wamegundua kuna shilingi milioni 155 hazijaonekana katika hati za malipo.

Sambamba na hilo alisema katika mradi huo unaonesha hakuna ushirikishwaji wa wananchi na wazazi kwa sababu waliagiza muktasari hawakupatiwa hivyo inaonesha hakuna vikao vilivyofanyika ambavyo vimewashirikisha wananchi.

Alisema Mwenge wa Uhuru utahitaji kupata taarifa ya uchunguzi kabla ya kuondoka katika mkoa wa Dar es Salaam, na kwa kusaidia TAKUKURU wamemkabidhi nyaraka ili kuanza kazi ya kutafuta thamani ya fedha na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.