- Kuna mabadiliko makubwa
- Huduma zote muhimu za jamii zote zinapatikana
- Sasa wanajenga mji mpya
- Kipindupindu sasa basi wanajenga na kutumia vyoo
Amina Ahmed , Maelezo, Pemba
NI Takriban dakika 15 kwa mwendo wa miguu na dakika tano kwa usafiri wa daladala au wa binafsi kutoka Madenjani hadi kufika katika barabara kuu iendayo bandari ya Likoni kuelekea kisiwa cha Kojani .
Eneo la Madenjani ni lango kuu la kuingilia na kutoka katika miji maarufu ya Kisiwa cha Pemba kama vile Chake Chake, Wete na Micheweni, ambapo barabara hiyo ndiyo ya kuelekea kisiwani humo.
SAFARI YA KOJANI
Ukiwa hapo Madenjani utaacha njia zote na kufuata barabara iendayo Micheweni, ndipo utakutana na bango kubwa linalokuashiria njia ya ndani ya kuelekea kisiwa cha Kojani.
Ni umbali wa dakika 10 hadi 20 kutoka bandari ya Likoni hadi kufika ndani ya kisiwa cha Kojani kwa kutumia vivuko vya majini ambavyo ni Ngalawa , Mashua, Dau au boti za kisasa za Faiba(fibres) , ambazo zote hazitumii mashine.
Kisiwa cha Kojani kipo nje kidogo na mji wa Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba na ni maarufu kwa shughuli za uvuvi na utamaduni wa kipekee wa watu wake wajulikanao kwa jina la “Wakojani”.
Ukiwa katika kivuko kuelekea kisiwa cha Kojani kwa fikira za haraka unaweza kuhisi kuwa kisiwa hicho hakina wakaazi wengi ndani yake , lakini kumbe ukweli haupo hivyo.
Muonekano unaokukaribisha kisiwani Kojani ni wa tofauti kutokana na baadhi ya nyumba nyingi za makaazi ya watu kuwa tafauti na kwengineko kisiwani Pemba.
Nyumba hizo zinaonesha haiba na muonekano wa kipekee katika ramani unayoiona na hasa kushonana sana na chochoro kama vile mji mkongwe wa Zanzibar, ila wao nyumba zao ni za chini.
Mandhari ya ujenzi wa kisiwa hicho unaweza ukadhani kwamba ni nyumba hizo zimehamwa au hazina uwezo wa kuhimili kukaa familia zaidi ya moja, lakini upekee wa wakaazi wa kisiwa hicho ni wa kushangaza.
Kwa vile nilikuwa na shauku na hamu ya kutaka kujua hali ya kisiwa cha Kojani na asili yake nilianza udadisi wangu kabla sijateremka kwenye chombo nilichopanda.
Kwa mujibu wa wenyeji wa kisiwa hicho walinisimulia kuwa asili ya jina la Kojani limetokana na neno “Kujini “ ambalo chanzo chake lilianza na mahojiano maalum kati ya wageni hao wa mwanzo ambao walikuwa peke yao kisiwani humo.
Watu wa mwanzo waliofika katika kisiwa cha Kojani nilisimuliwa kuwa waliwaona majini ndani ya kisiwa hicho na kujaribu kuzungumza nao kwa lugha zao, kwa majini kuuliza watu hao KUJINI wakiwa na maana ya kuwa“mumekuja kufanya nini “ na majini hao wakajibu “tujitukaa “wakiwa na maana ya kuwa tumekuja kukaa (kuishi) .
Kwa mujibu wa simulizi inaelezwa kuwa watu wa mwanzo walioingia ndani ya Kisiwa cha Kojani walikuwa ni wageni waliotokea sehemu za Iran, ambao idadi yao ilikuwa ni wanaume wawili waliojulikana kwa jina la Shah Kombo na Shah Simai.
Kwa vile wageni hao waliendelea kuishi katika kisiwa hicho walikuwa peke yao walilazimika kutafuta wanawake katika maeneo mbali mbali ikiwemo Kenya na kuja nao katika kisiwa hicho na kuanza kuzaa na kuzaana.
Vizazi hivyo viliendelea na wengine kujitokeza kutoka maeneo mbali mbali katika mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki ndipo walianza kubadilisha neno KUJINI mpaka kutamkwa ‘Kojani’.
Kisiwa hicho kwa sasa kina wakaazi zaidi ya elfu kumi na tatu (13,000), ambapo wapo wale ambao hawaishi katika kisiwa hicho wamehama kutokana na harakati za kimaisha, lakini ni zao la asili na ni ‘Wakojani’.
Kutokana na kukua kwa mji huo Serikali iliamua kufanya kisiwa cha Kojani kuwa ni wilaya ndogo ambayo huduma zote muhimu za kijamii zinapatikana katika kisiwa hicho, ambacho kwa ujumla kina shehia mbili shehia ya Kojani na shehia ya Mpambani .
WAKOJANI NA UCHUMI WA BULUU

Harakati kubwa za wakaazi wa kisiwa hicho kwa upande wa akina baba ni uvuvi, lakini kwa upande wa kina mama ni kilimo cha aina mbali mbali kama vile mpunga, mihogo, mtama na kadhalika kwa ajili ya chakula na sio biashara na ususi wa mikoba, mikeka, vipepeo na makawa kwa ajili ya biashara.
Kijana Bakari Hassan Bakari mwenye umri miaka 31, aliyezaliwa na kukua katika kisiwa cha Kojani , anasema tokea kuwa na fahamu zake yeye anajishughulisha na uvuvi wa samaki katika bahari ya Hindi na kazi hiyo alijikuta anairithi kutoka kwa baba yake mzazi.
“Mimi ni mvuvi na nimekulia katika shughuli hizi ambazo nimezirithi kidogo kidogo kutoka kwa baba yangu mzazi, nilipokuwa mdogo nilikuwa namfuata baharini mpaka nilipokuwa na mimi nishakuwa mzoefu hadi wakati huu sina harakati nyengine isipokuwa uvuvi”,alieleza .
Hata hivyo, Bakari anasema shughuli ya uvuvi kwa sasa zimekuwa na ugumu kutokana na kukosa nyenzo za kisasa za kuvulia, kwani kama unataka kupata samaki wenye kuingia sokoni lazima ufike kwenye bahari kuu ambako kuna hitaji zana za kisasa.
“Tangu awali mimi nakumbuka nilikuwa navua kupitia vyandarua nyavu za matundu madogo , mishipi ya ndoana na tulikuwa tunavua popote palipokuwa na bahari,lakini kwa sasa hali imebadilika ukivua kutumia nyavu ushakuwa na ugomvi na serikali kuna maeneo ukivua ushaingia mipaka ya hifadhi. Kwa kweli uvuvi sisi wakaazi wa Kojani kwa sasa umekuwa mgumu tunafanya kwa hayo hatuna kazi nyengine tu”, alisema.
Baadhi ya wazee ambao bado wanaendeleza harakati zao za kimaisha, kupitia makala haya wameiomba serikali kuwaandalia mazingira mazuri yatakayowasaidia wavuvi ambao hawatumii uvuvi wa bahari kuu, kuweza kufaidika na bahari kwa kuwasaidia na kuwapa elimu na mbinu za uvuvi unaotakiwa na serikali, ili kuendana na sera ya Uchumi wa Buluu.
“Sisi watu wa Kojani asili yetu ni uvuvi na serikali isione kwamba tukivua tunakosea ikatufunga au tukaanza kuwa mahasimu watutafute wavuvi wazungumze na sie, kama sisi tumefanya kazi ya uvuvi kwa urithi watupe izo mbinu za kisasa, lakini wanatoa maagizo tu hawatufiki wakatupa elimu na ndio maana ugomvi na serikali juu ya uvuvi haumalizi ‘’, alisema Mzee Mbarouk Hassan (Maarufu mzee makuti).
“Uchumi wa buluu sidhani kama umetuangalia sisi watu wa Kojani kwa sababu wavuvi wengi tunatumia bahari ya Hindi kuvua, leo serikali imewaza bahari kuu kwa hiyo si wote ambao harakati za uvuvi wanatumia bahari kuu,” alifahamisha akitamani kushirikishwa katika uvuvi wa kisasa.
Aidha aliongeza “Serikali kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu watuwekee Mkojani mwenye uzoefu na uvuvi kwa sababu wakazi wa Kojani ndio wavuvi, tumetapakaa ulimwengu nzima ambapo hata wazungu wanaiga tu kwa Mkojani, mbinu na uzoefu unaotusaidia ni kuonekana thamani ya mvuvi Tanzania mzima , lakini asiyejua uchungu na uvuvi, sifikirii kama kuna atakaeona umuhimu wa mvuvi ,’’.
Aliendelea kusema uvuvi hautaki kompyuta, bali unataka uzoefu kwa maana mtu akilala na kuamka akisikia mlio wa maji tu anajua leo baharini kunaendeka au hakuendeki, wakati kompyuta hazina akili za uvuvi kama uzoefu wa watu wa Kojani.
‘’ Serikali tunaiomba ije Kojani isikilize kilio chetu wavuvi wenye uzoefu, kama kweli imedhamiria kuenda kwenye uchumi huo wa buluu”, alisema Yussuf Salim Bakari.
Baadhi ya akina mama ambao wanajishughulisha na ususi wa mikoba mikeka na makawa walisema kazi hiyo na wao walirithi kutoka kwa wazazi wao .
“Mama yangu alikuwa ni mpakasaji maarufu wa mikeka na mikoba, na baba yangu ndio alikuwa muuzaji wake huichukua mikoba na mikeka kuvuka kwa kidau kuenda nayo mijini kuiuza na mimi kwa sasa naendeleza kazi hiyo ingawa mume wangu kuchukua kuenda kuuza haendi nalazimika kuchukua mimi mwenyewe kuenda nayo,” alisema Bi Time Mwiyaka wa Kojani.
Anasema kwa vile hana muuzaji wa uhakika sio mara nyingi kuenda nayo nje ya kisiwa cha Kojani, ila inanibidi ashone na kuiuza humo humo ndani, jambo ambalo linampunguzia soko.
Akizungumzia Soko la uhakika la kuuza bidhaa zao hizo wanazozalisha kwa mikono yao, anasema ndio limekuwa tatizo kwa sababu walianzishiwa kikundi hapo Kojani na aliegombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha NRA.
Alisema aliwaahidi kuwawezesha, lakini hakuwawezesha na wao uwezo wa kujiwezesha hawana kwa maana hiyo kikundi kikashindwa kuendelea kikafa mpaka leo.
Bi Time anawaomba wadau pamoja na serikali na wadau wa harakati za wanawake wawaangalie wanawake wa kisiwa hicho kwa kuwasaidia upatikanaji wa soko la biashara zao.
LAHAJA YA KIKOJANI
Baadhi ya Lafudhi halisi ya kisiwa cha Kojani kwa asieyekuwa mkaazi wa huko inataka umakini kuelewa ni kama zilivyo lafudhi nyengine za visiwa vidogo vidogo ikiwemo Tumbatu na maeneo mengine kama vile Micheweni.
Wakaazi wa kisiwa cha Kojani wana Lafudhi kama hizo ni kama unaweza ukasikia maneno kama ‘Kufisa’ ikiwa na maana ya kumsindikiza mgeni, ‘Kubauwa’ ikiwa na maana ya kujisaidia haja ndogo, ‘Kukeleshi’ ikiwa maana yake ni kukaa kitako.
Nyengine ‘Kudaukia’ hii nayo ikiwa na maana ya kujulia hali majirani,’
‘Kutongoa’ maana yake ni kuzungumza, na mengi mengineyo.
Hata hivyo, inasemekana wakaazi waliowengi katika kisiwa cha Kojani wana asili ya Kenya na Mombasa (Wagunya) kutokana na wale wanawake wa kwanza waliohamia walichukuliwa huko na ndio walioanzisha kizazi mpaka leo. Na hadi leo Wakojani hupendelea kufanya shughuli za uvuvi wakiwa huko nchini Kenya.
Aidha, utamkwaji wa lugha za mwambao kwa vizazi vilivyozaliwa kisiwani hapo na watu hao wa mwanzo zimekuwa ni maneno ya kujirudia rudia kwa vile ndio usuli wao.
KOJANI YA SASA
Zamani ukitaja neno Kojani wengi walikuwa walifahamu vyengine. Walikuwa na fikra kuwa wakaazi wa huko ni wakaidi na wasiopenda kubadilika.
Ni kweli ilikuwa hivyo, lakini Kojani ya leo sivyo ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita. Kumekuwa na mabadiliko makubwa na kuendena na cheo ilichopewa kisiwa hicho cha kuwa wilaya ndogo.
Katika kutembea yangu kisiwani humo nimegundua kuwa kisiwa hicho kina sehemu ya kale na ya sasa. Sehemu ya kale kuna nyumba zilizoshonana na chochoro na nyingi zimeezekwa makuti na ni nyumba duni zikionesha hali ya umasikini.
Hata hivyo, hali sio ilivyo hivi sasa, bali kuna mji wa kisasa unaojengwa kwa mpango na nyumba zake ni za matofali ya jasi zenye vyoo na pia vyumba vya ‘self contain’.
Kojani niliyokuwa nahadithiwa na nilivyoikuta ni tafauti kwa hivi sasa. Mara kadhaa kisiwa hicho kilikuwa kikikumbwa na maradhi ya Kipindupindu kutokana na wakaazi wake kujisaidia pwani na mazingira machafu, lakini hivi sasa wakaazi wana mwamko wa kujenga vyoo na kuvitumia na kuondokana na tabia ya zamani.Hata hivyo, matambara ya watoto kukoshwa pwani.
Hata hivyo, suala la taka bado linasumbua wananchi, kwa vile hakujakuwa na mpango madhubuti wa kudhibiti taka yaani ‘garbage management’.
Nilipowasogelea akina mama, niligundua kuwa wanafuraha hivi sasa kwa kuwepo Kituo chao cha Afya, ambacho huduma zote hivi sasa zikiwemo za kujifungulia wanapata hapo.
“zamani ilikuwa tunavuka tunaenda Likoni na Madenjani kwa huduma nyingi ikiwemo afya. Wengi tulikuwa tukijifungulia nyumbani”, alibainisha mwanamke mmoja huku akimuonea haya mwandishi wa makala haya.
Taarifa nilizozipata ni kwamba kituo chao hicho cha Afya kina madakatari wawili wanaokaa hapo na wengine wanakuja na kurudi na kwamba kimepunguza sana shida iliyokuwepo zamani ya kwenda Chwale.
Taratibu mwandishi wa makala haya alizunguka huku na kule na kujionea huduma nyengine muhimu zilizozmo katika kisiwa hicho, ambazo ni maji na umeme.
Kisiwa hicho hivi sasa kina umeme wa uhakika na pia maji safi na salama, vyote hivyo vimetoka nchi kavu na kwa kiasi kikubwa vimewaondolea usumbufu na dhiki kubwa wakaazi wa kisiwa hicho.
“Safari ya kuvuka kwenda Likoni na Madenjani kutafuta maji sasa hazipo. Twapata maji na umeme hapa hapa”, alifahamisha msichana mmoja.
Pitapita yangu kiswani humo nikakuta wakaazi wengi hivi sasa wana mawasiliano ya simu za mikononi, tafauti ilivyokuwa hapo nyuma, na nilipotupa macho huku na kule nikaona minara ya ya mawasiliano ya simu imejengwa kiswani na hakuna shida ya mtandao(network).
Huduma hii ya mawasiliano ya simu pia imesaidia sana kwa wakaazi wa kisiwa hicho, kupata huduma za kifedha kwa kupitia hiyo tafauti na hapo zamani.
Kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kisiwani humo, hivi sasa suala hilo halina usumbufu tena. Kuna usafiri wa kutosha na wa kisasa kwa kutumia boti za mashine na kuondokana na kutumia tanga.
Nilipodadisi zaidi usafiri nikaelezwa kuwa unatarajiwa kuimarika zaisi kwa kuwepo usafiri wa kisasa zaidi siku zijazo kwa kuletwa boti kubwa na ya kisasa. “Nasikia visiwa vyote vitapatiwa usafiri huo”, alidokeza sheha.
Suala la uzazi salama na mpango katika kisiwa hicho, nilidokezwa kuwa uzazi salama upo, kwani wengi wanajifungulia kituo cha afya hivi sasa.
Hata hivyo, uzazi wa mpango bado ni mtihani, kwani wanawake wanabeba mimba hata kabala yamuda wa kuachisha wa miaka miwili na uthibitisho ni kushuhudia watoto wa papo kwa papo tele.
Aidha, mabadiliko mengine kwa wanakojani hasa wanawake pia yapo husasan katika uvaaji wa nguo, kwani zamani ilikuwa zaidi kanga ya kifua kwa watu wazima na watoto kanga ya shingo, lakini kwa sasa wanajitanda vizuri na pia kuvaa mashungi.
Wa zamani waliosema jana haiwi leo hawakukosea, kwani katika kisiwa cha Kojani taratibu vijana wanabadilika na kuona mila na desturi za zamani zimepitwa na wakati,ambapo mila ya mwaka wa Kikojani hivi sasa hauna nguvu sana kama zamani.
“Vijana wanaona mambo haya yamepitwa na wakati na wa zamani ndio wanatoweka, basi ni hatari. Kilichobaki kwa sasa ni kuheshimu wakubwa. Hilo lipo hadi leo”, alisimulia sheha.
Kadhalika ngoma za asili nazo kisiwani humo nyingi zimekufa na vijana wanashuhgulika zaidi na muziki wa kisasa katika simu zao.
Juu ya hali wanawake wajane katika kisiwa hicho, mkaazi mmoja alidokeza kuwa mwanamke akiachika miiko yao haruhusiki kuishi katika nyumba peke yake ikiwa ni kuchelea kuingia katika maovu.
“Akiachika ntu nke hakai pekee bali arudi kwao na kukaa na watu. Si ruhusa kukaa pekee”, alifahamisha kijana mmoja.
CHANGAMOTO
Mara nyingi ndo za utotoni ni tatizo kwa jamii hasa katika jamii za vijijini. Suala hili kwa wakaazi wa Kojani limekuwa ni tatizo na bado hakujakuwa na mwamko wa kuleta mabadiliko.
Nilipodadisi ndoa za mapema nilielezwa kuwa tatizo hili lipo la wasichana kuozeshwa mapema. Jamii ya Wakojani inaamini kuwa msichana akifika miaka 15 aolewe, kwani ni umri muafaka na yasije yakatokea mengine.
Wanakojani wanaamini kuwa msichana akifika miaka 21 hajaolewa inakuwa ni nuhsi na kupata mikosi hapo baadae ya kukosa kuolewa.
“Mtoto wa kike akifika miaka 15 anastahiki kuposwa na kuolewa, ikizidi miaka 21 hajaolewa ni kama anaitia mikosi familia”, alisema bwana mmoja mzee.
Wazawa wa Kojani wametapakaa sehemu nyingi ikiwemo Kenya, Bara na Unguja. Hata hivyo, wana sifa kubwa ya kuthamini kwao na mara nyingi kuna baadhi ya misimu kurudi kwa wingi.