NA MWAJUMA JUMA

KAMATI ya nidhamu ya Chama cha Soka Mkoa wa Mjini Magharibi (UWERFA), imefuta uamuzi uliotolewa na kamati ya mashindano ya kushushwa madaraja mawili kwa klabu nne zilizohusika na upangaji matokeo.

Klabu hizo ni Kundemba FC, Muungano Rangers, Umoja ya Mbuzini na New City zilizokuwa zikisaka tiketi ya kucheza ligi daraja la kwanza kanda ya Unguja.

Kwenye michezo hiyo, Kundemba iliilaza Muungano Rangers magoli 31-0 nayo Umoja ya Mbuzini ikashinda 46-0 mbele ya New City.

Kwa mujibu wa barua ya kamati hiyo iliyotolewa Julai 30 mwaka huu na kusainiwa na mwenyekiti wake, Suleiman Said Suleiman, uamuzi wa Julai 20 wa kamati ya mashindano ya UWERFA kuhusiana na michezo hiyo umefutwa.

Hata hivyo, licha ya kupinga uamuzi huo, kamati hiyo ya nidhamu imeridhia kufutwa  matokeo ya klabu hizo na kupigwa faini ya shilingi milioni moja kwa kila timu ambazo zinatakiwa kulipwa si zaidi ya wiki moja.

Kamati hiyo, ilisema, adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kifungu namba 7 cha sura ya 22 ya kanuni ya mashindano ya mpira wa miguu Zanzibar.

Kwa mujibu wa barua hiyo, kamati kabla ya kutoa uamuzi huo kwa uwezo iliyopewa ibara ya 47(5) ya katiba ya UWERFA na katika kushughulikia kadhia hiyo, iliwaita na kusikiliza malalamiko kwa wahusika wote, Kundemba na Muungano  Rangers na kufuata ripoti za mwamuzi na kamisaa ambayo kila mmoja alitoa ushahidi wake.

Katika usikilizwaji wa kesi hiyo, kamati ilipata maelezo kutoka kwa Katibu wa Kamati ya Mashindano, Ibrahim Makeresa na Mwenyekiti wake, Ahmada Khamis ambao walisema kamati yao ilifikia uamuzi kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu namba tano cha kanuni ya kamati ya mashindano ya mkoa huo.