ZASPOTI
KOCHA Mkuu wa KMKM, Ame Msimu, amesema, kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Kagame ni matayarisho makuu kuelekea kwenye mechi zao za kimataifa.
KMKM ambayo itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imetinga hatua hiyo baada ya kuilaza Azam magoli 3-2 katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Alisema pamoja na kwamba wameshinda na kufikia hatua hiyo, lakini, wanahisi ni miongoni mwa maandalizi mazuri kwao ambayo yatawajenga wachezaji na kuwaweka tayari kwa michuano migumu ya Afrika.
Kocha huyo, alisema, mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Express ya Uganda unatarajiwa kuwa mgumu hasa kwa vile timu hiyo ina wachezaji wazuri.
“Ni moja ya timu nzuri na ina wachezaji wazuri, lakini, tutapambana licha ya kuwa utakuwa mchezo mgumu”, alisema.

Aidha, alisema, watatumia mchezo huo kuwaona wachezaji wao ni kwa namna gani wamekomaa na wanakwenda huku wakiwa na matumanini makubwa ya kushinda.
Alisema katika mchezo uliopita, waliwakosa wachezaji wake kadhaa akiwemo, Richard Jovit aliyemuia kifundo cha mguu na Salum Akida Shukuru, aliyeugua malaria ambao anatarajia kuwatumia kwenye mchezo wa nusu fainali.

“Kikosi kipo vizuri na wachezaji wote wapo sawa, wachezaji tuliowakosa sasa wapo vizuri na kureja kwao kutaongeza chachu ya ushindi”, alisema.
KMKM inatarajia kushuka dimbani kesho dhidi ya Express uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam majira ya saa 10:00.