NA MWANDISHI WETU

BAADA ya baadhi ya nwachezaji wa kikosi cha Simba kuondoka katika kambi ya timu hiyo na kurejea nchini mwao, kocha wa viungo Adel Zraine ameweka mkazo kwa wachezaji waliobaki wakiwemo Chris Mugalu, Bernard Morrison na Rarry Bwalya.

Samba iliyopo katika kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi kuu Tanzania bara na mashindano ya kimataifa nchini Morocco, baadhi ya nyota wake wamelazimika kuondoka baada ya kuitwa kwenye timu zao za mataifa yao.

Kwa mujibu wa Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wachezaji walioitwa katika timu zao za taifa wana majukumu ya kutimiza hivyo waliobakia wanaendelea na ratiba ya mazoezi kama ilivyoamuliwa na benchi la ufundi.

Rweyemamu alieleza kuwa Kocha Zraine amekuwa na programu maalum na wachezaji hao ili kuwaweka fiti kwa ajili ya msimu mpya wa 2021/22 ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

“Wachezaji ambao wameitwa timu zao za taifa lazima waendelee na majukumu yao huko walikoitwa, nasi tutaendelea kubaki na wale ambao wapo kambini kikubwa na kiujumla maandalizi yanakwenda vizuri na kila kitu kinakwenda sawa,” alisema Rweyemamu.

Kikosi hicho kinachotarajiwa kwenda marekani kabla ya kurejea nchini  kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea katika tamasha la Simba Day septemba 19 na mchezo wa ufunguzi wa ligi (Ngao ya Jamii) dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Septemba 25, mwaka huu.