LONDON, England
PEP Guardiola, ametangaza nia yake ya kuondoka Manchester City na kutafuta fursa katika kiwango cha kimataifa pindi mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu ujao.
Guardiola sasa yuko katika mwaka wa mwisho wa makubaliano yake kwenye Uwanja wa Etihad, ambapo amekuwa akifundisha tangu Julai 2016.

Baada ya kuchukua nafasi ya Manuel Pellegrini, bosi huyo wa zamani wa Barcelona ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu England, makombe ma ne ya EFL na Kombe la FA wakati wa enzi yake na ManCity.

Meneja huyo mwenye umri wa miaka 50, alisema, hana mpango wa kuongeza muda wa kubakia na klabu hiyo na kwamba analenga fursa na timu ya taifa.
“Baada ya miaka saba katika timu hii, nadhani itabidi nisimame”, alisema, katika hafla ya XP Investimentos.

“Nitalazimika kupumzika, angalia kile tumefanya, inavutia.”Na katika mchakato huu, ningependa kufundisha timu ya taifa, Amerika Kusini, Ulaya, kucheza Copa America, nataka kuwa na uzoefu huo”.

Lakini, Guardiola alizungumzia nafasi yake ya kumrithi Tite kama kocha mkuu wa Brazil.
Bosi huyo wa ManCity anahisi zao la sasa la nyota wa Brazil halitendewi haki ikilinganishwa na watangulizi wao wa zamani, lakini, anasisitiza watakuwa moja wapo ya wapendwa kwenye Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar. (AFP).