NA SABRA MAKAME, SCCM
AFISA Habari, Uhusiano na Masoko mpango wa Damu Salama Zanzibar, Ussi Bakar Mohamed, amewatoa hofu wananchi wanaohofia kuchangia damu kutokana na ugonjwa wa corona, kuondoa hofu hiyo kwani hawawezi kuambukizwa wala kuambukiza wengine.
akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Amani Kwa Wazee, Afisa huyo alisema wamebaini kuwa wananchi wanaogopa kuchangia damu kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya kuambukizwa corona wakati wengine wakidai kuwa kufanya hivyo ni chanzo cha kupoteza maisha na kizazi.
Alisema hali hiyo inatokana na uelewa mdogo walionao juu ya umuhimu kuchangia damu lakini pia maradhi mbali mbali ya kuambukiza ikiwemo corona.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kuchangia damu kwani mchangiaji mbali ya koukoa maisha yaw engine, hupata fursa ya kutambua afya yake baada ya uchunguzi,” alisema Ussi.
Aidha ussi alieleza kuwa kuchangia damu pia kuna faida kwa mchangiaji kwani baada ya kuchangia damu, mwili hujenga mfumo mzuri kwa kubadilisha seli zimezokomaa katika mwili wa binaadamu lakini pia kuepuka kuumwa na kichwa na uchovu wa mwili.
Pia alisema kuchangia damu humsaidia mchangiaji kujua afya yake na jinsi ya kujilinda na maradhi ambayo yanayotokana na upungufu wa damu na wingi wa damu.
Hata hivyo Ussi aliyataja makundi ya watu wasioruhusiwa kuchangia damu kuwa ni pamona na watu wanaotumia dawa za presha, kisukari, wagonjwa wa kifafa, wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwemo watumiaji wa madawa ya kulevya na ulevi kupindukia.
“Vigezo vyengine vya ziada vinavyomzuia mtu kuchangia damu hasa kwa wanawake ni kunyonyesha, mjamzito na mtu atakaekuwa kwenye siku za hedhi atahitajika kuchangia kabla ama baada ya siku tano kuingia au kutoka,” alisema.
Akizungumzia vigezo vya mtu kuchangia damu, Ussi alisema ni lazima mchangiaji awe amefikisha umri wa miaka 18 na uzito kuanzia kilogramu 50.
Afisa huyo alieleza kuwa changamoto kubwa wanayoipata ni kudharaulika na hata kukutana na maneno ya dharau katika jamii ambayo wamejipanga kuiondoa kwa kutoa elimu zaidi kuhusiana na uchangiaji wa damu.