KWA wakati huu macho na masikio ya walimwengu yameelekezwa nchini Afghanistan kuangalia upi utakuwa mustakbali wa nchi hiyo baada ya kundi la Taliban kuchukua madaraka.

Wakati dunia ikiiangazia Afghanistan kwa wakati huu na sisi anga za kimataifa hapa Zanzibar Leo, tumepiga kambi katika nchi hiyo tukijaribu kuchambua mawili matatu yanayoendelea nchini humo.

Katika makala haya tutaangalia kundi la Taliban ambalo limediriki kuchukua utawala nchini Afghanistan limetokea wapi na kundi la aina gani?

Kwa lugha ya Pashto inayozungumzwa sana nchini Afghanistanm Taliban maana yake ‘wanafunzi’, ambapo baadae walibadilika na kuwa vuguvugu la wapiganaji.

Kundi hilo lilijiongezea umaarufu na kuongezeka wanachama hadi kufikia hatua ya kitawala Afghanistan kuanzia mwaka 1996 hadi 2001, ambapo waliweka sheria za kiislamu.

Taliban ilikuwa ni moja wapo ya vikundi vinavyopigana vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Afghanistan katika miaka ya 1990 baada ya iliyokuwa Umoja wa Soviet kujiondoa nchini humo.

Taliban awali ilikuwa na wanachama kutoka kilichokuwa kikundi cha wapiganaji wa Afghanistan, maarufu mujahedeen, ambao walikuwa wakisaidiwa na Marekani wakati wakipigana na iliyokuwa Umoja wa Soviet katika miaka ya 1980.

Kikundi hicho kiliibuka tena mwaka 1994 katika eneo la kusini mwa Afghanistan katika mji wa Kandahar, ambapo muasisi wao alikuwa Mullah Mohammad Omar, Imam katika msikiti wa mjini humo, ambaye aliwaongoza wanamgambo hao mpaka alipofariki mwaka 2013.

Mullah Mohammed Omar, ambaye angekuwa mwanzilishi wa Taliban, alivunjika moyo kwamba sheria ya Kiislamu haikuwekwa nchini Afghanistan baada ya kumalizika kwa uvamizi wa Kisoviet.

Alikusanya wanafunzi 50 na kwa pamoja kundi hilo liliapa kuwaondoa wababe wa kivita na wahalifu, kurejesha utulivu, amani na usalama katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita.

Kikundi hicho kilikua kwa haraka, huku kikipata msaada kutoka Pakistan, na kuanza kuchukua miji na majimbo. Walikuwa maarufu kwa sababu walimaliza ufisadi na walifanya maeneo ambayo waliyadhibiti kuwa salama kwa biashara tena.

Taliban walipiga marufuku vitabu vya nchi za Magharibi na filamu na kuharibu vitu vya utamaduni vya tamaduni nyingine, ikiwemo masanamu makubwa yenye umri wa miaka 1,500 ya dhehebu la buddha katika bonde la kati la Bamiyan.

Mnamo 1996, walichukua udhibiti wa mji mkuu Kabul na kuipindua serikali. Kufikia 1998, serikali ya Taliban ilidhibiti asilimia 90 ya Afghanistan.

Taliban walitoa hifadhi kwa kundi la wanamgambo wa al-Qaida, lililokuwa wakati huo linaongozwa na Osama bin Laden.

Al-Qaida iliweka kambi za mafunzo nchini Afghanistan, ambako lilikuwa likiandaa mashambulizi ya kigaidi kote duniani, ikiwemo shambulizi la Septemba 11, 2001 nchini Marekani.

Chini ya mwezi mmoja baada ya mashambulizi ya Septemba 11, Marekani na washirika wake waliivamia Afghanistan. Mapema Disemba, serikali ya Taliban ilianguka, na Marekani ilianza kufanya kazi na raia wa Afghanistan kuunda serikali ya kidemokrasia.

Kufuatia kushindwa dhidi ya uvamizi wa Marekani viongozi wa Taliban walikimbilia kwenye ngome zao kusini na mashariki mwa Afghanistan au upande mwingine wa mpaka nchini Pakistan.

Kundi la wanamgambo baadae liliongoza uasi dhidi ya serikali mpya ya Afghanistan iliyokuwa ikiungwa mkono na Marekani, wakitumia mabomu waliyotengeneza wenyewe na mashambulizi ya kujitoa muhanga.

Kuna mfumo wazi juu ya uongozi ndani ya kundi la Taliban, ambapo kwa sasa  Mawlawi Hibatullah Akhundzada amekuwa kiongozi mkuu wa kundi hilo tangu 2016.

Akhundzada ni msomi wa kidini mwenye mamlaka kuu katika masuala yote ya kisiasa, dini na kijeshi katika kundi hilo.

Kiongozi huyo anaungwa mkono na manaibu watatu na mawaziri kadhaa ambao husimamia vitengo vya kijeshi, ujasusi na uchumi.

“Rahbari Shura,” anayejulikana pia kama “Quetta Shura,” ndiye mwenye mamlaka ya juu zaidi ya ushauri wa kundi hilo lenye washirika 26.

Tawi la kisiasa la Taliban ambalo linaliwakilisha kundi hilo kimataifa liko mjini Doha, nchini Qatar, ambapo masuala ya siasa yanaongozwa na mwanzilishi mwenza wa Taliban Mullah Abdul Ghani Baradar.

Uwepo wa tawi la kiasa la Taliban nchini Qatar ni sehemu ndogo tu ya kundi hilo ambapo kazi yake kubwa ni kusimamia na kuratibu mazungumzo ya amani na Marekani.

Kundi hili la wapiganaji linapata pesa nyingi kupitia usafirishaji wa mihadarati na dawa ya aina ya opium na heroin. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa mnamo 2018 na 2019 pekee, Taliban walipata zaidi ya dola milioni 400 kupitia biashara hii haramu ya dawa za kulevya, ambayo inachukua hadi asilimia 60 ya mapato ya kundi hilo.

Aidha ripoti ya Hanif Sufizada mchambuzi wa sera za uchumi katika kituo cha mafunzo cha Afghanistan amesema Taliban wana vyanzo vya ziada vya mapato ambavyo ni pamoja na madini, ushuru na michango. Inadhaniwa kuwa nchi nyengine pia hulifadhili kundi la Taliban kifedha.

Guido Steinberg, kutoka Taasisi ya Ujerumani ya masuala ya kimataifa na usalama (SWP), alikaririwa akisema kuwa Taliban wana washirika wawili, mmoja ni mshirika asiyeonekana na Iran.

Walinzi wa Mapinduzi nchini Iran wanadaiwa kuunga mkono Taliban katika miaka ya hivi karibuni ili kuwashinda Wamarekani, mshirika wao wa pili na muhimu zaidi ni Pakistan.

Mnamo mwaka 2020 serikali ya Marekani ilifanya mazungumzo kufikia makubaliano na Taliban baada ya zaidi ya miongo miwili ya kuhusika kijeshi nchini Afghanistan.

Makubaliano hayo yaliweka ratiba kwa wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini humo kwa maelewano ya kuacha kuwashambulia Wamarekani na kuingia katika mazungumzo na serikali ya Afghanistan.

Lakini, miezi ya mazungumzo kati ya Taliban na serikali ya Afghanistan yalishindwa kufanikisha makubaliano yoyote ya amani.