DAMASCUS, SYRIA

KUNDI la wanaume wenye silaha kutoka mkoa wa kusini wa Daraa wa Syria walihamishwa hapo juzi kutoka maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi kaskazini mwa Syria chini ya makubaliano ya wapatanishi wa Urusi ili kupunguza mvutano wa miezi mingi, shirika la habari la serikali SANA liliripoti.

Jumla ya wanaume wenye silaha 45 na wengine wakiwa na familia zao walipakiwa kwenye mabasi kuelekea kaskazini mwa Syria baada ya kukataa kuwa chini ya mamlaka ya Syria huko Daraa, ilisema ripoti ya SANA.

“Uokoaji huo ni sehemu ya mpango wa kurejesha usalama huko Daraa”, ilisema.

Wakati huo huo, Uchunguzi wa Haki za Binadamu wa Syria ulisema kuwa watu hao wenye silaha ambao walihamishwa Alhamisi walikuwa kundi la pili.

Ilisema viongozi wa Syria walitaka watu 100 wenye silaha kuondoka Daraa kuelekea maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi kaskazini mwa Syria.

Mnamo Agosti 24, mkataba wa saa 48 ulianza kutumika Daraa kujiandaa kwa uokoaji wa watu hao wenye silaha. Polisi wa jeshi la Urusi waliingia vitongoji katika eneo la Daraa al-Balad kujiandaa kwa uokoaji.

Kufuatia kuondoka kwa kundi hilo, taasisi za serikali ya Syria zitarudi Daraa wakati wa juhudi zikifanywa ili kuwezesha kurudi kwa maelfu ya watu waliokimbia eneo hilo.

Ofisi ya UN ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) hivi karibuni iliweka idadi ya wakimbizi wa ndani katika eneo la Daraa al-Balad na maeneo ya karibu katika mkoa huo kuwa imefikia watu 38,600, wakiwemo wanawake 5,000 na zaidi ya watoto 20,400.

Jeshi la Syria liliingia Daraa mnamo mwaka 2018 baada ya waasi kutengwa kwenye maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi katika mkoa wa Idlib kaskazini magharibi.