NA MADINA ISSA

KATIBU wa Chama cha nage mkoa wa Kusini Unguja, Mohamad Ali Manzi, amesema wataendeleza kukuza mchezo huo kwa kushiriki mechi mbalimbali, zinazoandaliwa katika sherehe za kiserikali na kichama ili kuona mchezo huo unaimarika.

Akizungumza na Zanzibar leo katika maonesho ya tamasha la Kizimkazi, linaloendelea kufanyika katika kijiji hicho, katibu huyo, alisema kwa upande wao wamekuwa wakicheza sehemu mbalimbali ikiwemo maeneo ya kiutalii.

Aidha alisema  mchezo wa nage kwa Zanzibar upo rasmi na  umesajiliwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hivyo, alisema wapo tayari kushiriki kama walivyokuwa wakishiriki mwanzo pamoja na kuingia katika matamasha mbalimbali yanayofanyika, ili kuweza kukuza mchezo huo wa nage katika mkoa wao.

Aidha alifahamisha kuwa nage iliyokuwepo hivi sasa sio nage ya zamani ya kujaza chupa, lakini ya sasa imekuwa na kanuni shehia zipatazo 160 ambazo zimeandaliwa katika chama cha michezo Zanzibar.

Hivyo, alitumia nafasi ya kuwakaribisha wannachi kwenda kuangalia mchezo wa nage katika tamasha la Kizimkazi liloandaliwa na Benki ya CRDB.

Sambamba na hayo, alimpongeza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, kwa ushirikiano wake juu ya mchezo huo.

Nae, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusisnao wa Benki ya CRDB Tuully Esther Mwambapa, alisema tamasha la Kizimkazi, linaendelea katika kijiji cha Kizimkazi na kilele chake kinatarajiwa kufanyika Agosti 28 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Aidha alisema mbali na mchezo wa nage kutakuwa na mchezo wa mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mbio za baskeli, resi za ngalawa, michezo ya wanafunzi wa maandazi pamoja na maonyesho ya sana na ngoma ya  shomoo.