NA MUHSIN ALI (SCCM)
KATIBU wa klabu ya KVZ Academy Fc Khamis Abdul-Hamid Hamid amesema, lengo la kuanzishwa timu za vijana limefikiwa kwa kiasi kikubwa na zimekuwa msaada kwenye timu za wakubwa.
Alisema wamekuwa wakipata shida kununua wachezaji, hivyo uwepo wa timu hizo kumesaidia kupata vijana watakaoipigania timu kwa muda mrefu.
“Tuna haja ya kuwa na timu za vijana kutokana na kanuni za ligi zinatupasa kufanya hivyo”, alisema.
Aidha ameeleza kuwa bado kumekuwa na uhaba wa fedha za uendeshaji wa klabu, jambo ambalo limewakwamisha katika kutimiza baadhi ya majukumu yao.
Sambamba na hayo alisema, licha ya vikwazo mbalimbali vinavyojitokeza, bado wanapambana kuwasaidia vijana wadogo wenye vipaji katika mchezo wa soka.
Amewataka wadau pamoja na taasisi binafsi kuwaunga mkono katika jitihada zao za kuendelea kuibua vipaji.
Kwa upande wake nahodha timu hiyo ambaye tayari amepandishwa kwenye timu kubwa Rashid Hamid Shindano amesema, kupata nafasi ya kuwepo kwenye timu hiyo, ni jambo ambalo linalowapa faraja vijana na kuwaongezea ari ya kufika mbali.
Pia amewataka vijana wenye vipaji kuchangamkia fursa zinazowazunguka kimichezo ili kujiepusha kujiingiza kwenye makundi maovu.