UMOJA wa Kujihami wa nchi za magharibi (NATO), ulianzishwa mnamo mwaka 1949, baada ya kumalizika kwa vita vya pili vya dunia, ambapo nchi zilizojiunga na umoja huo zilikubaliana kuungana kwenye masuala ya ulinzi na usalama.
Ulianza na wanachama 12, lakini hadi kufikia sasa NATO ina wanachama 30, ambapo wengi wa wanachama hao ni nchi za barani Ulaya na wanachama wengine ni nchi za Marekani na Canada.
Moja ya jukumu kubwa na muda mrefu la NATO ni kuhakikisha linaidhibiti Urusi, ambayo inaonekana kama kitisho kikubwa sio tu kwa nchi za Ulaya, lakini hata kwa Marekani na washirika wake waliopo sehemu mbalimbali duniani.
Mara kadhaa NATO na Urusi zimekuwa zikirushiana vita vya maneno, huku wakati mwengine pande hizo zikiekeana misimamo mikali inayotishia kukaribia kuingia vitani.
Katika wakati huu inaonekana upepo umeanza kubadilika kidogo kwani China imejumuishwa kwenye orodha ya mataifa yenye kuitia hofu NATO na kutokana na hali hiyo mkutano wa kilele wa mwaka huu mjadala wa NATO ulihusu kitisho cha China dhidi ya umoja huo.
Kwanini NATO inaifuatilia China? Kwa mujibu wa taarifa NATO ilisema nia na tabia ya China imeonesha changamoto za kimfumo katika sheria za kimataifa zilizowekwa na katika maeneo ambayo yanahusiana na usalama wa pamoja.
Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo wa siku moja mjini Brussels, viongozi wa NATO wameelezea kwa matamshi makali wasiwasi wao kuhusu tabia za China wanazosema zinakwenda kinyume na maadili ya jumuiya hiyo pamoja na sheria za kimataifa.
Wasiwasi mkubwa ulioelezwa na mataifa wanachama wa Jumuiya hiyo ni pamoja na kuimarika kwa uwezo wa kijeshi wa China, uhusiano kati ya nchi hiyo na Urusi pamoja na kile walichokitaja kuwa kukosekana uwazi mjini Beijing.
Katibu mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo kuwa NATO haitaki kuingia kwenye vita baridi na China kwani China sio wapinzani wao wala maadui zao.
Jens Stoltenberg aliongeza kusema kuwa NATO inapaswa kuwasilisha hisia zake kwa sasa na kujua kuna changamoto ya kukua kwa China kuwa tishio la usalama.
China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika uimara wa jeshi na kukua kwa uchumi, ambapo chama tawala nchini humo cha kikomunisti kinahusisha sana siasa, maisha ya kila siku na katika jamii kwa ujumla.
China kwa sasa inaongoza kwa kuwa na jeshi kubwa zaidi duniani, ambapo taifa hilo la mashariki ya mbali lina wanajeshi zaidi ya milioni mbili waliopo kazini.
Nato imeanza kuwa na wasiwasi wa kuongezeka kwa uwezo wa jeshi hilo la China, ambalo linaonekana kuwa tishio katika usalama na miiko ya demokrasia katika wanachama wake.
Aidha taarifa zinaeleza kuwa NATO imekuwa na wasiwasi mkubwa na hatua za China kuimarisha uwezo wake wa kinyuklia pamoja na urafiki wake wa kijeshi wa karibu mno na Urusi.
Katika miaka ya hivi karibuni, muungano huu umeongeza hofu ya shughuli ambazo China inazifanya barani Afrika, ambako wameweka kambi wakitekeleza miradi mbalimbali ya kimikakati ikiwemo ujenzi wa miundombinu.
Katika mkutano huo wa viongozi wa NATO, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema kwenye suala la China, hadhani kwama kuna mtu anataka vita vipya baridi na taifa hilo.
Naye rais wa Marekani, Joe Biden alisema Jumuiya ya NATO ni sharti isimame imara dhidi ya kitisho kinachoongezeka kutoka Beijing na Moscow.
Biden akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari pamoja na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, ameikosoa tabia ya Urusi na China.
“Tumetambua katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kwamba tunakabiliwa na changamoto mpya, inayotokana na Urusi ambayo imekuwa na mienendo ambayo hatukuitarajia na mienendo ambayo hata China inaikumbatia,” alisema Biden.
“Maadili ya demokrasia yaliyo kitovu cha ushirika wetu yanakabiliwa na mbinyo wa ndani na wa nje. Urusi na China zote zinajaribu kuukaba koo mshikamano wetu wa magharibi. Lakini ushirika wetu ni msingi imara ambao tunaweza kuutumia kujenga ulinzi wa pamoja na ustawi imara”, alisema Biden.
Kuangaziwa zaidi kwa China kunatokana na hisia za Joe Biden ambaye anashiriki kwa mara ya kwanza kama rais wa Marekani, lakini wanachama wengine, husasan nchi za ukanda wa Baltiki zinazopakana na Urusi, bado zinaichukulia Moscow kama kitisho kikubwa zaidi kwa usalama wao.
Lakini ni rahisi kuitenga China kimataifa kama NATO inavyotaka? Licha ya matamshi makali yaliyotolewa kuhusu China, viongozi kadhaa wa mataifa ya Jumuiya ya NATO walisema bado ni muhimu kushirikiana na Beijing katika masuala mengi ikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Biden mwenyewe ni miongoni mwa wale wanaoamini kuwa siyo rahisi kuitenga moja kwa moja China katika uga wa kimataifa.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema China, taifa kubwa na lenye nguvu za kiuchumi duniani ni hasimu kwenye maeneo mengi, lakini wanakubali kuwa Beijing bado ni mshirika muhimu katika masuala chungunzima.
Beijing yenyewe inasemaje kufuatia kuzungumzwa na kushutumiwa sana katika mkutano wa NATO? China imeishutumu NATO kwa kusema mambo ya uongo kuhusu maendeleo ya amani.
Katika majibu yake, China ilitaja sera yake ya ulinzi ni ya kiuhalisia na kuitaka NATO kutotumia nguvu nyingi katika kuhamasisha mijadala isiyo na faida.
“Uimara wa ulinzi na jeshi letu kuwa la kisasa ni suala ambalo linaweza kuthibitshwa kwa kuangalia uhalisia, uwazi, uwajibikaji na sababu zinazopelekea kuwa hivyo,” China iliandika mpango huo katika taarifa yake kwa Umoja wa Ulaya.
Aidha ilieleza NATO inapaswa kuangalia maendeleo ya China katika mpangilio mzuri na kuacha kuchukua maslahi na haki halali ya China kwa minajili ya kisiasa katika mataifa mbalimbali, kuweka malumbano na kuchochea ushindani.