NA MWAJUMA JUMA

KOCHA Mkuu wa Mafunzo, Said Kwimbi, amesema, umasikini wa klabu ndio unaochangia kutokuwa na nguvu kubwa ya kudhibiti wachezaji kuachana na michuano ya ndondo.

Hayo aliyaeleza alipozungumza na mwandishi wa habari hizi, ambapo alisema wachezaji wengi wanakwenda kwenye ndondo kutokana na kufuata fedha ambazo hupatiwa baada ya mchezo.

Alisema, hali hiyo pia  inapelekea hata baadhi ya wachezaji kukimbia katika timu zao na kwenda kucheza mechi za ndondo.

“Hii kwa sababu hatuna ufadhili wa kutosha, kama mchezaji unamlipa vizuri anaweza kuacha, kwa kujua kwamba hiyo ndio ajira yangu kwa hiyo hatokuwa tayari kwenda kucheza mechi yoyote ya ndondo”, alisema.

Kocha huyo, alisema, kutokana na hali hiyo wachezaji wamekuwa wakipunguzwa viwango vyao vya uchezaji, kwa kukosa muda wa kupumzika.

“Utakuta mchezaji ametoka mazoezini katika klabu yake, lakini, jioni anakwenda kucheza ndondo na pengine hana timu moja anayoichezea, kesho yamle yamle, kesho coconut anajikuta anachoka hata akija katika klabu yake hafanyi vizuri”, alisema.