ZASPOTI
KLABU ya Leicester City imebeba taji la kwanza msimu huu, ikiifunga Manchester City goli 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii ikiwa ni sehemu ya ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu ya England.

Goli pekee kwenye mchezo huo liliwekwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria, Kelechi Iheanacho kwa mkwaju wa penalti kufuatia mlinzi wa kati wa ManCity, Nathan Ake kufanya madhambi eneo la hatari.
Pambano hilo lilipigwa uwnaja wa Wembley.

ManCity pamoja na kumtumia kiungo mshambuliaji ghali England, Jack Grealish, haikufanikiwa kusawazisha na kuanza vibaya msimu huu.
Mbali na kosa kosa za Ilkay Gundogan na mshambuliaji wa Leicester, Jamie Vardy bado matokeo yalibakia kuwa na faida kwa kocha Brendan Rodgers ambaye amekuwa na wakati bora tangu kutua viunga vya King Power.

Kocha wa ManCity, Pep Guardiola, alikuwa amezungumza kabla ya kuanza kwa mchezo huo juu ya kuwa na wakati mdogo wa kujiandaa na msimu mpya huku ‘nusu ya timu’ kuwa nje.
Nyota wakubwa wenye maumivu walikuwa, Kevin de Bruyne na Phil Foden ambao waliumia wakati wa michuano ya Ulaya msimu wa joto, na Raheem Sterling pia aliachwa nje huku vijana wasio na uzoefu, Cole Palmer (19), na Sam Edozie (18), wakianzishwa.

Rodgers, akizungumza na BBC Radio Leicester: alisema: “Kulikuwa na hisia nzuri kuja hapa. Kila mchezaji wa Leicester, shabiki, mfanyakazi akija hapa, ilikuwa hisia ya kipekee.
“Tulitaka kulipeleka hilo kwenye mchezo na kuendelea kuwa na hisia, na tunashukuru tumefanya hivyo.”
Kwa upande, Guardiola, alisema: “Hongera Leicester. Nimeridhika zaidi na jinsi tulivyocheza. Vitu vingi vilikuwa vizuri, wachezaji wachanga walikuwa bora.
“Tulipata dakika kwa wachezaji kwa ujumla, mambo mengi mazuri.”

Leicester wameshinda mchezo wao wa kwanza dhidi ya Manchester City nje ya michuano ya ligi tangu ushindi wa 4-3 kwenye Kombe la FA mnamo Februari 1968, wakiwa hawajashinda katika mechi 12 kwenye michezo kama hiyo kabla ya juzi.(BBC Sports).