NA ABDI SULEIMAN
MWAKILISHI Viti Maalumu kupitia Wasomi Kisiwani Pemba Lela Mohamed Mussa, amekabidhi vifaa mbali mbali vya michezo kwa klabu zilizomo ndani ya jimbo la Ole.
Alitoa kauli hiyo wakati alipokua akizungumza na wanamichezo wa mpira wa miguu na vikundi vya mazoezi, katika hafla ya kukabidhi vifaa vya michezo huko uwanja wa mpira Ole Kipangani wilaya ya Chake Chake.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuunga mkono mikakati ya Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi katika kuinua sekta ya michezo.
Alisema katika kumuunga mkono Dk. Mwinyi, amelazimika kutoa vifaa hivyo, ili kuwafanya wanamichezo kuendelea kufanya mazoezi pamoja na kucheza mpira, ikizingatiwa kuwa mpira sasa ni ajira.
Mwakilishi huyo ambaye ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, alisema kwa sasa kilio kikubwa cha wanamichezo hao kimetatuka, kwani vifaa hivyo wataweza kuvitumia katika shughuli zao za michezo.
“Kama tunavyojua kwa sasa mpira ni ajira kubwa duniani, katika kutekeleza ahadi na mikakati ya rais wetu tumeona tukabidhi vifaa hivi vya michezo kwanza ili kuona vijana wanacheza mpira na kufanya mazoezi” alisema.
Akitoa neno la shukurani kiongozi wa kikundi cha mazoezi Kidike Fitness Club Dk.Hasnuu Faki Hassan, alisema msaada huo umekuja kwa wakati muafaka, huku akimpongeza Mwakilishi huyo kwa msaada huo.
Katibu wa timu ya Sawazisho Hamad Salum Sharif, alisema vifaa hivyo vimefika katika wakati muafaka, kwani vitawasaidia kwenye mazoezi pamoja na kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ya ligi.
Naye Shaame Farahan Khamis alisema wamefarajika sana baada ya kupatiwa vifaa vya mazoezi ya viungo, huku akimpongeza mwakilishi huyo kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa kwao.