Salum Vuai
WAKATI akiingia madarakani baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, hakuna sekta aliyoiacha katika vipaumbele vyake, akija na mikakati madhubuti ya kuziletea maendeleo nyanya zote.
Bila shaka, michezo ni miongoni mwa sekta ambazo Dk. Mwinyi anaziangalia kwa jicho la tatu, kwani hafichi kueleza namna anavyosononeshwa jinsi Zanzibar ilivyopoteza hadhi katika michezo mbalimbali ambayo miaka ya nyuma iliiletea sifa.
Mpira wa miguu kwa hapa Zanzibar ambao ndio unaokusanya kundi kubwa la mashabiki, kwa takriban miongo miwili sasa umekosa kuwapa mashabiki ladha wanayoitarajia, na hivyo kupoteza mapenzi kwa klabu za hapa kwao na kujichagulia timu zinazocheza ligi za nje hasa bara la Ulaya.
Ingawa hakuna rekodi kubwa za kujivunia kwa klabu za Zanzibar na timu zetu za taifa za wachezaji wa umri mbalimbali kutwaa ubingwa kwenye mashindano ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na yale ya Afrika, lakini kiwango cha wachezaji wetu kilikuwa tishio kwa timu za nchi jirani.
Hata hivyo, bado tunazo kumbukumbu za timu yetu kubwa ya Taifa Zanzibar Heroes, kutwaa ubingwa wa Challenge mwaka 1995 katika ardhi ya ugenini nchini Uganda, pamoja na ubingwa wa vijana chini ya miaka 20, ambapo timu yetu Karume Boys iliutia mikononi katika uwanja wa Amaan mwaka 2003.
Zanzibar ina historia kubwa ya kutoa wachezaji wenye vipaji vizuri, ambavyo vilizishawishi klabu kongwe Tanzania, Yanga na Simba kuvitupia macho na kuvisajili kwa ajili ya kuzitumikia katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Aidha, vipaji hivyo vilizikuna pia klabu nyengine za ligi hiyo, kama vile Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting, Azam FC na Coastal Union, ambazo zilitenga fedha kwa ajili ya kusajili wanandinga kutoka Zanzibar.
Kwa kuwa Mhe. Rais Dk. Mwinyi aliikuta hali ya soka katika kipindi kigumu cha kuporomoka na kunuia kufanya kila njia ili kurejesha vuguvugu lake, wapenzi wa mchezo huo nchini walipata matumaini makubwa kuwa hilo litawezekana na kuwasahaulisha vipindi vya majonzi.
Hata hivyo, nikiwa miongoni mwa wapenzi wakubwa wa soka ambaye nina shauku kuona timu za Zanzibar zinafika mbali, ninasikitishwa na hali inayoendelea sasa kisiwani Pemba.
Wasiwasi wangu, kama tatizo hilo halitatafutiwa dawa mapema, dhamira ya Rais na matumaini ya Wazanzibari kuhuisha soka, zitashindwa njiani.
Kutokana na mgomo unaoendelea sasa kwa timu za Pemba kususia kutia mguu viwanjani kutafuta timu ya kuiwakilisha katika Ligi Kuu msimu wa 2021/2022, Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) linashindwa kupanga ratiba na kutangaza tarehe ya kuanza mashindano hayo ya kusaka bingwa wa visiwa hivi.
Tayari timu zitakazocheza ligi hiyo kutoka Unguja zimeshajulikana huku mchakato ukikwamishwa na mgomo wa wenzao wa Pemba ambao wanatakiwa kutoa timu moja ili kukamilisha idadi ya 12 kuwezesha kuanza kwa michuano hiyo.
Inasikitisha kuwa mpaka sasa wakati mwaka 2021 ukiwa umevuka nusu ya kwanza na kuelekea mwisho, bado Pemba inaendeleza msuguano na ZFF ikidai utaratibu wa kupata timu za kucheza Ligi Kuu ubadilishwe, kwa kila kisiwa kuwa na ligi yake na kupatikana wawakilishi wa Ligi Kuu kama ilivyokuwa ikifanyika zamani.
Mimi sitaki kujiegemeza upande wowote, si timu za Pemba wala ZFF kwa vile sina maslahi kokote, lakini ninaamini jambo hilo linaweza kuzungumzwa kwa busara, ufumbuzi ukapatikana na ligi ikachezwa bila mivutano.
Kwa maoni yangu, kinachohitajika kuweka mambo sawa, ni kuwepo MARIDHIANO yatakayopatikana kwa vikao kati ya uongozi wa Wizara dhamana ya michezo, BTMZ, ZFF na timu zinazodai mabadiliko na hata zilizokwishafuzu kucheza Ligi Kuu.
Bila ya jitihada za kuleta maridhiano kufanyika huku tukiendelea kusubiri wanaogoma wagomoke, ifahamike kwamba mwaka utakatika na hakuna ligi itakayochezwa na hivyo kuikosesha Zanzibar wawakilishi wa michuano ya Afrika mwakani.
Kama tutashindwa kupata muafaka kwa mazungumzo, itabidi tufanye dua ya kuwaombea wanaogoma wabadilishe msimamo wao huo kwa maslahi mapana ya soka la Zanzibar maana hapo itahitajika kudra ya Mwenyezi Mungu tu kukipindua chuma kilichopinda.
Simu: 0777 865050/0714 425556
Baruapepe: mbumbwinihalisi@gmail.com