TUMEKUWA tukiyasikia maagizo ya msisitizo yanayotolewa na viongozi wa juu nchini Tanzania kila pale wanapopata fursa ya kuagana ama kuzungumza na mabalozi wetu wanaotuwakilisha nchi za nje.

Kwa bahati nzuri viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata wale wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, maagizo wanayowapa mabalozi wetu yamekuwa yakifanana.

Si maagizo mengine bali viongozi hao huwataka mabalozi wahakikishe wanazingatia na kuitekeleza kivitendo diplomasia ya uchumi ambayo dhamira yake kubwa ni kwa muinufaa ya nchi ya Tanzania.

Hakuna shaka hivi sasa diplomasia duniani imebadilika kwa kiasi kikubwa, sio ile ya mabalozi kwenda kuwawakilisha nchi za nje na kuzungumza mahusiano na mashirikiano.

Diplomasia ya sasa sio kuvaa koti kubwa, tai yenye kuburura chini, ama kila siku kuingia kwenye mikutano isiyo na tija wala faida zaidi ya kupiga makofi na kutikisa kichwa kwamba kilichozungumza kimekuingia.

Mabadiliko ya diplomasia kwa jinsi yalivyobadilika wakati mwengine yanamlazimisha balozi ama maofisa wa ubalozi kuvua makoti na kuingia mzigoni kuinadi nchi yetu juu ya fursa mbalimbali zilizopo.

Kwa bahati nzuri kama kuna fasaha wa kuieleza diplomasia ya uchumi kwa lugha rahisi na nyepesi, ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.  Hussein Ali Mwinyi.

Kwa tunavyoelewa Tanzania na Zanzibar yapo maeneo mengi ambayo hayajaguswa hasa kiuwekezaji, hata yale yaliyoguswa bado zipo fursa nyingi ambazo ziko wazi kabisa hata kipofu anaona.

Kwa tunavyoelewa biashara hasa mazao ya kilimo ya kiwemo ya biashara na matunda baina ya nchi yetu na maeneo mengine ya dunia, bado haijashamiri kiasi cha kuwanufaisha wakulima wetu.

Aidha nchi yetu ambayo imejaaliwa kuwa na vivutio vya kipekee duniani vya utalii, ikiwemo visiwa vya Zanzibar, bado havijaweza kutangazwa nje ya nchi na kuweza kuongeza mapato nchi yetu.