ATHENS, UGIRIKI

MAELFU ya watu wanaopinga kupigwa chanjo wameandamana katika miji miwili ya Ugiriki wakilalamikia masharti makali yaliyotangazwa kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Miongoni mwa sheria mpya ni kwamba watu ambao hawakuchanja hawatoruhusiwa kuingia mikahawani na kuanzia Septemba mosi wahudumu wa afya ambao waliogoma kuchanjwa watafukuzwa kazi bila ya malipo.

Vyombo vya habari vimekisia kwamba watu wapatao 3,000 waliandamana mjini Athens na wengine zaidi ya 5,000 waliandamana katika mji wa kaskazini wa Thessaloniki.

Karibu na maandamano hayo kumalizika mjini Athens, watu wapatao 200 walianza kuwarushia mawe polisi nje ya jengo la bunge.

Polisi waliwatawanya kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi, na maji ya kuwasha.Serikali ya Ugiriki ililazimika kutangaza masharti makali kwani maambukizi yaliongezeka hivi karibuni kutokana na kwamba ni kipindi cha likizo barani Ulaya.