BRASILIA, BRAZIL

MAHAKAMA ya Juu nchini Brazil imeanzisha uchunguzi dhidi ya rais wa nchi hiyo kwa kutuma kwenye mitandao ya kijamii nyaraka za uchunguzi wa siri wa polisi.

Jaji Alexandre Moraes aliamuru kuwa Rais Jair Bolsonaro achunguzwe kwa kuziweka hadharani nyaraka ambazo zilikuwa zinahusiana na uchunguzi wa polisi juu ya kudukuliwa kwa mahakama ya uchaguzi.

Udukuzi huo ulifanyika miezi kadhaa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2018, ambapo Bolsonaro anasema alizituma mtandaoni kuthibitisha hoja yake kuwa mfumo wa uchaguzi unaweza kufanyiwa ubabaishaji.

Jaji Moraes alimuamuru Rais Bolsonaro kuzifuta nyaraka hizo mtandaoni na pia kuondolewa kwa Ofisa wa polisi aliyeongoza uchunguzi huo.

Kupitia matangazo yake ya kila wiki mtandaoni, Bolsonaro alisema kuwa nyaraka hizo zinapaswa kuwapo hadharani kwa kuwa ni jambo lenye maslahi ya umma.