KINSHASA, DRC

MAKUMI ya watu wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea huko magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kapteni wa Polisi ya DRC, Antoine Pululu aliliambia shirika la habari la AFP kuwa, watu wasiopungua 33 walifariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia Jumapili magharibi mwa nchi.

Alisema moto mkubwa ulizuka baada ya lori la mafuta kugongana ana kwa ana na basi lililokuwa limejaza abiria kupita kiasi katika kijiji cha Kibuba, umbali wa kilomita 80 kutoka mji mkuu Kinshasa.

Ofisa mwengine wa polisi katika eneo hilo alisema miili ya wahanga wa ajali hiyo iliteketezwa na moto hadi kubakia majivu, na kwamba mabaki yaliyopatikana yalizikwa.

Idadi kubwa ya watu hupoteza maisha katika ajali za barabarani kila mwezi nchini DRC kutokana na kupindukia kasi, magari mabovu, kubeba abiria na mizigo ziada na hali mbaya ya barabara.

Oktoba mwaka 2018, watu 53 walifariki katika ajali nyengine iliyohusisha lori la mafuta katika moja ya barabara kuu za kuelekea Kinshasa.Mwaka 2010, watu 230 walifariki dunia baada ya lori jengine la mafuta kupinduka nchini DRC.