NA MADINA ISSA
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Maryam Mwinyi, leo anatarajiwa kufungua Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival) ambapo zaidi ya wajasiriamali 300 watashiriki tamasha hilo linalofanyika katika mwambao wa pwani ya Kizimkazi, mkoa wa Kusini Unguja.
Tamasha hilo la siku tano linatarajiwa kuinua uchumi wa watu wa mkoa wa Kusini Unguja pamoja na majirani wa mkoa huo.
Baada ya kuzinduliwa kwa tamasha hilo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo maonesho ya wajasiriamali watakaonesha bidhaa na huduma mbali mbali wanazotoa zinazokwenda sambamba na malengo ya uchumi wa buluu.
Aidha katika kutunza mazingira na kuweka vijiji vya Kizimkazi katika hali ya usafi kutakua na usafi wa mazingira ya fukwe na vijiji.
Akizungumza na mwandishi wa Zanzibar leo, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kiserikali na Mawasiliano kutoka Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa alisema benki hiyo imetoa udhamini wa zaidi ya milioni 300 ili kufanikisha tamasha hilo.
Alisema mbali na udhamini huo pia wana mpango wa kuubadilisha na kuupa hadhi mkoa wa Kusini Unguja kwa kudhamini miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa kituo cha maegesho ya gari za abiria, masoko, vituo vya afya na skuli.
Aidha Mwambapa alisema pia wana mpango wa kutoa elimu ya ujasiriamali na biashara kwa wananchi wa mkoa huo ili kuinua vipato vyao.
Alisema lengo la CRDB ni kulifanya tamasha hili kuwa endelevu, lenye kutangaza vivutio mbalimbali vya Zanzibar, kuchochea utunzaji wa mazingira na kutoa fursa za kiuchumi kwa wana Kizimkazi.
“Kizimkazi ina utajiri mkubwa wa vivutio vya kiutalii ikiwemo fukwe nzuri, hoteli za kisasa, dolphins, tamaduni na historia ya Kizimkazi yenye kuvutia wengi, hivyo kupitia matangazo yetu mbalimbali mtaona na kusikia hazina kubwa ilioko Kizimkazi,” alieleza Tully.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, alisema tamasha hilo litakua na vyakula vya asili na kuwaomba watakaoshiriki tamasha hilo kuwaunga mkono wajasiriamali hao kwa kununua vyakula vya asili.