Ni kwa kushindwa kutekeleza jukumu la usafi
NA KHAMISUU ABDALLAH
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesitisha mkataba na kampuni ya usafishaji ya GREEN WASTE GROW, kwa kile kilichoelezwa kwamba kampuni hiyo imeshindwa kutekeleza majukumu ya kusimamia usafi wa mazingira katika mji wa Zanzibar.
Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Mjini, Suleiman Mohammed Rashid, aliyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Malindi Mjini Unguja.
Alisema kilichosababisha serikali kusitisha mkataba na kampuni hiyo, ni kushindwa kusimamia suala la usafi katika maeneo waliyokubaliana kwa mujibu wa mkataba wao.
Aidha alisema walikuwa wakipokea maelekezo mbalimbali kutoka wizarani juu ya kampuni hiyo na kupewa muda kufanya mabadiliko juu ya huduma wanayoitoa kutokana na kukithiri kwa taka nyingi ndani ya majaa hasa maeneo ya mjini.
“Baada ya muda waliopewa hakukuwa na matokeo chanya ndipo wizara ikatupa muongozo wa kukaa pamoja baina ya uongozi wa manispaa na kampuni na kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa”, alisema.
Alifahamisha kuwa mambo yote hayo ni kuona lengo la serikali linafikiwa katika usafi wa mji kama dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwa mji wote unakuwa safi na kuwa kivutio kwa wageni wanaoingia nchini hasa watalii.
Alisema baraza hilo liliingia makubaliano ya mkataba na kampuni hiyo Disemba mwaka jana baada ya kukamilika kwa taratibu za manunuzi na mashauriano kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
Alifahamisha kuwa, mkataba huo ulihusisha ufanyaji wa kazi katika maeneo ya Baraza la Manispaa ambayo yalihusishwa maeneo makuu matatu ikiwemo eneo la Mji Mkongwe, Magharibi na Kusini huku Manispaa ikiendelea kusimamia eneo lao la Kaskazini.
Alisema miongoni kwa kazi za msingi za kampuni hiyo ni kuhakikisha inafanya usafi katika maeneo hayo waliyopangiwa, kushughulikia masuala ya mitaro, kusimamia bustani na kusimamia tozo zinazotokana na huduma ya usafi katika maeneo yaliyotengwa.
Aidha alisema kampuni hiyo ilianza kazi rasmi Disemba 1 mwaka jana ambapo ndani ya kazi zake inazozifanya ililazimika Baraza la Manispaa Mjini kujenga mashirikiano ya karibu.
“Wakati kampuni hii inaanza kazi ilitumia vifaa vya Baraza la Manispaa Mjini lengo letu ni kuhakikisha kazi inafanyika vizuri ya kuweka mji katika hali ya usafi,” alibainisha
Mbali na hayo, alisema Baraza lilitenga siku moja ya kila wiki kwa kutengeneza timu maalum yenye lengo la kukaa na uongozi wa kampuni hiyo ili kuona kasoro na changamoto zinazojitokeza kwa madhumuni ya kuzipatia ufumbuzi.
“Lengo letu ni kuona kampuni hii inaweza kufanya kazi na kufikia malengo ya serikali kuu ya kuona Mji wa Zanzibar na maeneo yake yote unakuwa safi wakati wote,” alisema.
Kaimu huyo, alisema sambamba na kazi hizo kampuni hiyo walikaa vikao kupitia ngazi mbalimbali juu ya huduma wanayoitoa lakini pia kutoridhishwa na mfumo mzima wa taka
Aidha alisema ziara aliyoifanya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi Februari 27 mwaka huu aliguswa na usafi wa mji ambao ulikuwa unafanywa na kampuni hiyo na kufanya maamuzi ya kutengua eneo moja la Kusini kuwa miongoni mwa maeneo ambayo yalikuwa yakisimamiwa na kampuni hiyo.
Alisema lengo la Rais kutengua eneo hilo ni kuona kampuni hiyo inakwenda sambamba na vifaa walivyonavyo na huduma wanayotakiwa kuitoa na kupatikana kwa ufanisi wa kazi wanayoifanya.
“Baraza letu liliendelea kutoa mashirikiano ya karibu sana kuhakikisha kwamba kampuni hii inaweza kuendelea kutoa huduma ndani ya Baraza la Manispaa Mjini,” alisema.
Shaaban, alifahamisha kuwa Mei 13 mwaka huu Meneja wa kampuni hiyo aliyekuwepo Zanzibar pamoja na yeye walipokea wito kutoka wizarani ambao uliwataka kukaa pamoja ili kusikiliza na kuangalia changamoto zilizokuwepo.
“Ndani ya kikao hicho kampuni ile ilipewa wiki moja kufanya mabadiliko juu ya huduma wanayoitoa kutokana na kukithiri kwa taka nyingi ndani ya majaa hasa ya mjini na kutoa tahadhari endapo kama watashindwa kubadilika katika suala la usafi basi hatua zitachukuliwa kwa kupunguzwa eneo jengine,” alisema.
Alisema Baraza la Manispaa lilitoa onyo kwa kampuni hiyo juu ya dhamira ya kutengua eneo moja kati ya mawili waliyokuwa nayo.
Alisema Baraza la Manispaa lilifuata taratibu zote za kuondoka kwa kampuni hiyo ambazo zimo ndani ya vipengele vya mkataba wa makubaliano.
“Tulisema pale ambapo hatutaweza kuridhishwa na huduma basi tutaweza kutengua ama kuvunja mkataba jambo ambalo tuliweza kulizingatia hilo baada ya kupata ushauri kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuonekana kampuni hiyo ilivunja vipengele muhimu vya mkataba,” alisema.
Mbali na hayo, alibainisha kwamba kampuni hiyo ilitakiwa kurejesha asilimia 20 ndani ya Manispaa baada ya makusanyo na kutoa gharama zao yaliyoainishwa ndani ya mkataba na baada ya kutaka kupunguzwa eneo moja walionesha kutokuwa tayari kurejesha asilimia hiyo.