NA ZUHURA JUMA

MAHAKAMA ya Mkoa Wete, imeiahirisha kesi inayomkabili mshitakiwa Makame Khamis Hamad,25, mkaazi wa Kijichame  aliedaiwa kubaka kutokana mashahidi kutofika mahakamani.
Mara baada ya mshitakiwa kupanda kizimbani akisubiri taratibu za mahakama, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Mohamed Ali Juma, alidai shauri hilo lipo kwa ajili ya kusikilizwa lakini hawajapokea mashahidi.

“Mheshimiwa hakimu shauri hili lipo kwa ajili ya kusikilizwa lakini hatujapokea mashahidi, hivyo tunaiomba mahakama yako tukufu kulipangia
tarehe nyengine,” alidai.

Hakimu wa mahakama hiyo, Abdalla Yahya Shamhun, alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kusema kuwa shauri hilo litarudi tena mahakamani Septemba 1 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

“Nimeliahirisha kesi hili hadi Septemba 1 mwaka huu, hivyo mashahidi waitwe ili siku hiyo tuwasikilize,” alisema.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 25 mwaka huu saa 2:00 usiku Kijichame kwa Pengo wilaya ya Micheweni ambapo alimbaka mtoto mwenye miaka 16, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 108 (1) (2) (e) na kifungu cha 109 (1) vya sheria nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya
Zanzibar.

Wakati huo huo, Juma Mohamed Juma,18, mkaazi wa Makangale anaekabiliwa na shitaka la kumuingilia msichana mwenye miaka 17,
amefutiwa dhamana baada ya kutohudhuria mahakamani kwa zaidi ya mara mbili.

Kesi ya mshitakiwa huyo imekuwa ikiahirishwa kila ilipoitwa kwa sababu mshitakiwa hafiki mahakamani.

Hakimu wa mahakama ya Mkoa Wete, Abdalla Yahya Shamhun, aliifuta dhamana ya mshitakiwa baada ya kupuuza wito wa mahakama.

Baada ya mshitakiwa kupanda kizimbani, Wakili wa serikali, Mohamed Ali Juma alidai shauri hilo lipo kwa ajili ya utetezi.

Hata hivyo, mshitakiwa alipoulizwa alidai kwamba hayupo tayari kuanza kujitetea kwa sababu hali yake sio nzuri.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Semtemba 1 mwaka huu kwa ajili ya utetezi.

Ilidaiwa mshitakiwa, alitenda kosa hilo Novemba 11 mwaka 2019 saa 9:00 za jioni Makangale wilaya ya Micheweni.

Ilidaiwa bila halali alimuingilia msichana mwenye miaka 17 huku akifahamu kwamba ni
mulemavu wa akili.