NA ABOUD MAHMOUD

MASHINDANO ya mchezo wa soka kwa timu za mashirika, kampuni na taasisi mbali mbali za serikali na binafsi, yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 28 mwaka huu.

Akizungumza na Zanzibar Leo muandaaji wa mashindano hayo Abdullah Thabit (Dulla Sunday), alisema michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa katika dimba la Mao Zedong majira ya usiku.

Muandaaji huyo alieleza kwamba mashindano hayo yatajulikana kwa jina la ‘Dulla Sunday Cup’.

Alisema michuano hiyo inatarajiwa kuchukua muda wa mwezi mmoja yana lengo la kuwaweka wafanyakazi pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar katika kuhamasisha michezo.

“Lengo langu la kuandaa michuano hii ni kuwaunganisha wachezaji wa soka kutoka katika taasisi mbali mbali za serikali na binafsi pamoja na kuunga mkono juhudi za Dk. Mwinyi katika kuhamasisha michezo”, alisema.

Alisema kwa sasa bado mapema kuyataja mashirika yatakayoshiriki mashindano hayo, ambapo alifahamisha kwamba baadhi ya washiriki bado hawajarudisha fomu.

Sambamba na hayo Sunday alifafanua kwamba katika michuano hiyo wanatarajia bingwa kuondoka na zawadi ya shilingi 1,000,000 na mshindi wa pili 500,000.