NA ADELADIUS MAKWEGA ,WHUSM
SERIKALI imekipongeza Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA), kwa kuanzisha mashindano ya ‘Miss &Mister Deaf Tanzania’ ambayo yanayotarajiwa kufanyika Septemba 2021.
Akizungumza ofisini kwake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mfaume Said alisema mashindano hayo washindi watakaopatikana watashiriki mashindano kimataifa ya viziwi.
“Kuna vijana na warembo wengi wenye sifa zote kwa ndugu zetu viziwi, hili ni jambo jema na wizara tukishirikiana na KISUVITA maandalizi ya msingi yamekamilika.”alisema.
Akitoa maelezo ya mashindano hayo Hadija Kisubi ambaye ni Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo alisema ni mara ya kwanza kufanyika mashindano hayo.
“Kama alivyozungumza Kaimu Mkurugenzi wetu Sanaa, mashindano haya yanatarajiwa kufanyika Septemba 14, 2021 katika ukumbi wa Serana Dar es Salaam.”
Akizungumzia mashindano hayo Habibi Mrope ambaye ni Mkurugenzi wa KISUVITA alisema hapo awali waliomba msaada kutoka kwa wadau wengine lakini zoezi hilo liligonga mwamba.
“Lakini tulipowasiliana na wizara yetu jambo hili limekuwa jepesi na limeungwa mkono kwa asilimia 100 na sasa sisi kama KISUVITA tunatembea kifua mbele na hatua za mwisho za kukamilisha mashindano haya zimeshafikiwa’’
alisema.
Washindi wanne watakaopatikana katika mshindano hayo wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika na baadaye ya Dunia yatakayofanyika Aprili mwakani huko Brazili.